1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano mapya yaibuka kati ya Israel na Palestina

12 Aprili 2022

Mapigano mapya yameibuka kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Palestina katika mji wa Jenin wakati raia mmoja wa kipalestina alipomchoma kisu polisi wa Israel kabla ya kuuwawa kwa kupigwa risasi.

Israel l Protest der jüdischen Extremistengruppe "Lahava" in Jerusalem
Picha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Kijana huyo wa kipalestina alimchoma kisu afisa mmoja wa Israel wakati wa operesheni ya ukaguzi katika mji wa Ashkelon, hali iliyosababisha polisi kumuua kwa kumpiga risasi.

Mshambuliaji huyo aliye na umri wa miaka 40 anasemekana kutokea mji wa Hebron ulioko Palestina kusini mwa Ukingo wa Magharibi. Afisa aliyechomwa kisu alipata majeraha madogo.

Israel bado inaendeleza siku ya nne ya operesheni ya kulinda doria karibu na mji wa Jenin baada ya mshambuliaji katika mji huo kuwapiga risasi na kuwauwa watu watatu katika baa moja mjini Tel Aviv wiki iliyopita.

Soma zaidi:Jeshi la Israel ladaiwa kutekeleza mauaji Ukingo wa Magharibi

Usiku wa kuamkia leo Waziri Mkuu Naftali Bennett aliitembelea baa hiyo iliyofunguliwa tena huku akionya kuwa Israel haitokubali maadui wao kusitisha maisha ya watu wake na kuapa kupambana nao bila kuchoka.

Wakaazi:Mapigano yalitanguliwa na mirindimo ya risasi

Huku hayo yakiarifiwa wakaazi wa Jenin wameliambia shirika la habari la AFP kwamba vurugu hizo mpya zimetokea baada ya ufayatulianaji wa risasi uliofanyika katika siku za hivi karibuni.

Polisi wa Israel wakitumia maji ya kuwasha kutawanya watuPicha: Ammar Awad/REUTERS

Nalo shirika la habari la Palestina Wafaa limeripoti mapigano hayo kuzuka kati ya vijana wadogo wa kipalestina na wanajeshi wa Israeli walipoanza kushambuliana baada ya wanajeshi wa Israel kutumia risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi dhidi yao. Jeshi la Israel halijasema lolote kuhusu tukio hili.

Soma zaidi:Mzozo wa Israel waripuka katika mkutano wa kilele wa AU

Hali katika eneo hilo imekuwa tata baada ya mashambulizi manne yanayodaiwa kufanywa na wapalestina kusababisha vifo vya waisraeli kadhaa ndani ya wiki mbili.

Israel yahofia ghasia zaidi

Israel inahofia kutokea kwa ghasia zaidi wakati huu ambako waumini wa kiislamu wako katika mfungo wa Ramadhani ulioanza mwanzoni mwa mwezi Aprili, na kabla ya sikukuu ya wayahudi na pasaka kwa waumini wa kikristo.

Polisi wa Israel mpakani wakiwazuia baadhi ya raiaPicha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Mwaka uliopita vurugu mjini Jerusalem zilisababisha mapigano ya siku 11 kati ya Isral na wanamgambo wa Hamas wanaousimamia Ukanda wa Gaza.

Soma zaidi:Ripoti ya Shirika la Amnesty International imeitaja Israel kuwa ni taifa linalozingatia ubaguzi wa rangi

Aidha Wapalestina pamoja na makundi ya kutetea haki za binaadamu wanadai jeshi la Israel linatumia nguvu kupita kiasi na mara nyengine linawajeruhi na kuwauwa watu ambao hawana hatia.

Wajumbe wa kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya Palestina wameishutumu Israel pia kutumia nguvu kupita kiasi kuwadhibiti vijana wa kipalestina.

Chanzo: Mashirika

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW