1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano mapya yaripotiwa Mashariki mwa Congo

28 Septemba 2017

Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umetuma majeshi yake mashariki mwa nchi hiyo kufuatia mapigano mapya yaliyotokea huko.

Beni Demokratische Republik Kongo Blauhelmsoldaten 23.10.2014
Picha: Alain Wandimoyi/AFP/Getty Images

Umoja huo wa Mataifa haukufafanua ni wanajeshi wangapi waliopelekwa Kivu Kusini, Mashariki mwa Congo kwa sababu ya wasiwasi wa kimkakati. Kutokana na kupunguzwa kwa bajeti, tume ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa, Monusco walilazimika kufunga baadhi ya maeneo yake Mashariki mwa Congo mapema mwaka huu.

Hata hivyo msemaji wa jeshi la Congo amesema kwa siku kadhaa sasa, wanajeshi wamekuwa wakipambana na wanamgambo karibu na mji wa Uvira mpakani na Burundi. Kapteni Dieudonne Kasereka hakutoa maelezo mengine yoyote juu ya majeruhi. Makundi mengi ya wanamgambo yanafanya kazi zake Mashariki mwa Congo wakipigania maeneo yaliyotajiri kwa rasilimali ya madini. 

Huku hayo yakiarifiwa jeshi la wanamaji lilipambana na wanamgambo katika ziwa Tanganyika. Mapigano hayo kati ya wanamgambo wa Mai Mai Yakutumba na vikosi vya serikali ya Congo yalianza mapema wiki hii nje kidogo ya mji wa Uvira karibu na mpaka wa Burundi. Hali ya wasiwasi imezidi kuongezeka tangu Rais Joseph Kabila alipokataa kuondoka madarakani baada ya muda wake kumalizika Desemba mwaka uliopita.

"Tangu saa kumi na moja asubuhi kumekuwepo na makabiliano ya risasi kati ya jeshi na wanamgambo wa Mai Mai mjini Uvira," alisema Lubungula Dem's M'Sato, mwanachama wa kundi la kutetea amani mjini Uvira, mji wa pili kwa ukubwa katika mkoa wa Kivu Kusini.

Jeshi lawarudisha nyuma wapiganaji

Kwa upande wake msemaji wa jeshi Louis-Claude Tshimwanga amesema jeshi la Congo pia limefanikiwa kuwasogeza nyuma wanamgambo hao waliokuwa katika maboti ziwani Tanganyika, huku akitoa hakikisho kwamba vikosi vya serikali bado vinadhibiti eneo la Uvira. Ziwa Tanganyika lina urefu mkubwa na kupakana na Burundi, Tanzania na Zambia.

Kambi ya wakimbizi ya Warundi ya Lusenda, Kivu Kusini, katika fukwe za ziwa TanganyikaPicha: MONUSCO/Abel Kavanagh

"Wanamgambo walijaribu kuushambulia mji wa Uvira kupitia ziwa Tanganyika, walikuwa na maboti yaliyokuwa yanakwenda kwa kasi," alisema mtu mmoja aliyeshuhudia kisa hicho ambaye hakutaka jina lake litajwe, akiongeza kuwa aliona maboti sita ya wanambambo hao. Amesema jeshi la wanamaji lilifanikiwa kukamata boti moja kati ya hayo sita. Aidha Mai-Mai Yakutumba, waliundwa mwaka 2007 na mwanamgambo mmoja aliyenyimwa nafasi ya kujishirikisha katika jeshi la kitaifa la Congo. Kundi hilo pia limeanzisha kundi kubwa la wafanyibiashara haramu wa madini ya dhahabu karibu na Ziwa Tanganyika.

Wiki hii katika taarifa iliyowekwa katika mitandao ya kijamii kiongozi wa kundi hilo la wanamgambo  William Yakutumba amesema vikosi vyake vinapinga kile walichokiita matumizi mabaya auusimamizi mbaya wa rasilimali asilia za nchi na kushindwa kuachia madaraka baada ya kipindi chake kikatiba kumalizika.  Maeneo yaliyotajiri kwa madini Mashariki ya Congo yamekuwa yakikumbwa na vita vya kikabila na kwa zaidi ya miongo miwili Congo imekubwa na machafuko yaliyosambaa nje ya nchi.  Eneo hilo la Mashariki mwa Congo ni mzalishaji mkubwa wa ,madini ya Cobalt inayotumiwa katika simu na vifaa vyengine vya elektroniki.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/reuters

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW