Mapigano na mauaji zaidi nchini Syria
12 Oktoba 2012Katika tukio hilo la leo asubuhi waasi sita pia waliuwawa kwenye kizuizi kimoja cha kijeshi katika eneo la Khirba. Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu nchini Syria pia limesema kwamba kwa sasa mapigano yanazidi kupamba moto katika miji ya kaskazini Idlib na Aleppo.
Shirika hilo lililo na makao yake makuu jijini london, awali lilitoa taarifa kwamba jana Alkhamisi kulishudiwa mapigano makali zaidi kuwahi kutokea nchini Syria, tangu kuanza kwa ghasia miezi 19 iliopita, ambapo watu 240 waliouwawa wakiwemo wanajeshi 92, waasi 67 na raia 81. Kati ya wanajeshi waliouwawa hapo jana 36 waliuwawa katika mapigano mjini Idlib. Mji huu umeshuhudia ghasia zaidi katika miezi mitatu iliopita.
Hii leo ndege mbili za kivita za utawala wa Rais Bashar Al Assad zilishambulia majengo mawili katika mji wa Idlib tangu waasi walipoushikilia mji huo baada ya mapambano makali na vikosi vya serikali kwa takriban saa 48. Kulingana na mkurugenzi wa shirika hilo la kutetea haki za binaadamu Rami Abdel Rahman, waasi walikishambulia kikosi cha jeshi la anga katika barabara kuu inayounganisha mji wa Allepo na Raqa.
Akizungumza na shirika la habari la AFP kwa njia ya simu, Rami alisema shambulizi kati ya waasi na jeshi la anga lililoanza usiku wa manane lilidumu hadi asubuhi. Uwanja wa ndege wa majeshi imekuwa ikilengwa mara kwa mara na waasi nchini Syria kwa kuwa wametoa ndege zaidi za kivita kushambulia upinzani.
Tangu mapigano kuanza nchini Syria miezi 19 iliopita watu zaidi ya 32,000 wameuwawa.
Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle anatarajiwa kuzuru Uturuki siku ya Jumamosi kuzungumzia ghasia ya nchini Syria. Taarifa zaidi kutoka balozi ya Ujerumani Westerwelle atakutana na waziri mwenzake Ahmet Davutoglu mjini Istanbul.
Ziara hii imekuja wakati Uturuki ililazimisha ndege moja ya abiria ya Syria iliokuwa imetoka Urusi kuelekea Damascus kutua katika uwanja wa ndege wa Uturuki kwa madai kuwa ilikuwa imebeba silaha, jambo ambalo utawala wa Syria umelikanusha.
Mwandishi Amina Abubakar/AFP
Mhariri Mohammed Khelef