Mapigano ya Armenia-Azerbaijan yapamba moto
1 Oktoba 2020Kupitia taarifa ya pamoja iliyotolewa na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Vladimir Putin wa Urusi na Donald Trump wa Marekani, viongozi hao wametaka kukomeshwa mara moja kwa uhasama kati ya vikosi vya majeshi ya nchi hizo mbili.
Ufaransa, Urusi na Marekani kwa pamoja zinaongoza kundi linalojulikana kama OSCE Minsk ambalo kwa miaka kadhaa limeratibu juhudi za kutafuta suluhu ya mzozo wa jimbo Karabakh bila kupata mafanikio. Soma pia: Rais Hassan Rouhani aelezea wasiwasi kuhusu mzozo wa Nagorno-Karbakh
Lakini katika hotuba kwa bunge la Uturuki kabla tu ya kutolewa taarifa hiyo ya nchi tatu, Rais Tayyip Erdogan alisema anapinga kuhusika kwao "Ikizingatiwa kuwa nchi tatu za kundi la Minsk, Marekani, Urusi na Ufaransa zimepuuza tatizo hili kwa karibu miaka 30, haikubaliki kuwa zinahusika katika kutafuta usitishwaji mapigano katika wakati huu ambao matukio yamejitokeza katika siku za karibuni na kama kuna kitu kinatakikana, wavamizi wanapaswa kuondoka ardhi hiyo ili kupatikana suluhu."
Amesema mpango wa kudumu wa kuwekwa chini silaha unaweza kufikiwa tu kama Waarmenia watajiondoa eneo la Nagorno Karabakh.
Mapigano makali kati ya Armenia na Azerbaijan juu ya jimbo hilo linalozozaniwa yalizuka Jumapili iliyopita na hadi sasa yamesababisha mauaji ya kiasi watu 130 huku makabiliano bado yakiendelea.
Wanahabari wawili wa Ufaransa na wawili wa Armenia wamejeruhiwa leo katika eneo la Nagorno-Karabakh.
Ikulu ya Urusi imesema Rais Putin mapema leo aliujadili mzozo huo na Baraza la Usalama la nchi yake. Putin na Macron pia walijadili jinsi kundi la OSCE Minsk linavyoweza kusaidia kusitisha mapigano hayo. Soma pia: Azerbaijan yatangaza kuuwawa kwa raia wake 10 kutokana na mapigano
Urusi pia imejitolea kuwa mwenyeji wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Armenia na Azerbaijan kwa mazungumzo ya kumaliza mapigano hayo.
Duru ya serikali ya Ujerumani imesema viongozi wa Umoja wa Ulaya watauzingatia mzozo huo katika mkutano wa kilele mjini Brussels baadaye leo
Reuters, dpa, ap