Mapigano ya Armenia na Azerbaijan yauwa 59
28 Septemba 2020Mapigano makali zaidi kutokea katika kipindi kirefu, kati ya Armenia na taifa jirani la Azerbaijan yameendelea ambapo leo hii yameingia siku yake ya pili kwa kufyatuliana makombora. Mapigano hayo ya sasa ambayo yamesababishwa na mzozo wa jimbo la Nagormo-Karabakh kwa leo yanatajwa kugarimu maisha ya wanaotaka kujitenga 28.
Eneo hilo la Nagormo-Karabakh, ambalo kimataifa linatambuliwa kama sehemu ya Waislamu wa Azerbaijan, limekuwa likidhibitiwa na kundi la waliojitenga la Waarmenia kwa miongo kadhaa, huku kukiwa na makuabiliano tete ya amani tangu miaka ya 90. Jeshi la Azerbaijan limedai kufanikiwa kuyakomboa maeneo kadhaa ya kimkakati ya milima ya Nagorno-Karabakh.
Vifo vilivyotokea kwa upande wa Armenia
Aidha limeongeza wapiganaji wa wanaotaka kujitenga 28 wameuawa katika mapigano ambayo yametokea leo na kufanya idadi jumla ya waliuwawa kufikia watu 59. Viongozi wa mataifa kadhaa wamezitaka nchi hizo kuacha mapigano, baada ya mengine mabaya zaidi kutokea 2016 ambayo yanaashiria vita vipya kati ya mataifa hayo ambayo yalikuwa sehemu ya uliokuwa Umoja wa Kisovieti.
Mataifa hayo yamekuwa katika mkwamo wa mgogoro wa kimipaka, tangu kipindi hicho cha miaka ya 90, pale ambapo Karabakh ilipojitangazia uhuru wake, baada ya vita ambayo iligharimu maisha ya watu 30,000. Hata hivyo hakuna hata taifa moja ambalo liliutambua Uhuru wa Karabakh. Lakini hadi sasa Azerbaijan haijatoa taarifa za vifo vilivyotokea kwa upande wa jeshi lake, tangu kuzuka kwa mapigano haya ya sasa. Ufaransa, Urusi na Marekani zilishiriki jitihada za upatanishi kwa kile kilichofahamika kama "Kundi la Minsk" lakini jitihada kubwa kabisa ya mwisho ilivunjika 2010.
Soma zaidi:Mapambano yazuka kati ya majeshi ya Armenia na Azerbaijan
Wakati huo huo Rais Racept Tayyip Erdogan wa Uturuki ameitaka Armenia kuliachia eneo la la Nagorny Karabakh baada ya kuzuka kwa mapigano hayo, katika eneo la mpakani la Azerbaijan. Amenukuliwa na shirika la habari la Ufaransa AFP akisema "Umewadia muda kuufikisha kikomo mgogoro huo ambao ulitokana na ukaliaji wa Nagorny Karabakh, na kwamba Armenia ikiondoka tu, mgogoro huo utakuwa umekwisha."
Uhispania nayo haijakuwa nyuma katika mzozo huo, ambapo waziri wake wa masuala ya kigeni Arancha Gonzalez alionesha kusikitishwa na hayo yanayotokea na kutoa wito wa kusitishwa mapigano wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
Vyanzo: AFP/DPA/RTR