1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mapigano ya Kinshasa yanatia wasiwasi"

Maja Dreyer22 Agosti 2006

Udondozi wa magazeti wa leo hii ni wa mchangayiko - siyo tu wa maoni tofauti, kama kawaida, bali pia ni mchangayiko wa masuala husika.

Tunaanza hapa nchini Ujerumani, ambapo Kansela Angela Merkel jana alitoa hotuba yake ya kwanza baada ya likizo ya majira ya joto. Wahariri wengi lakini hawakuridishwa na maneno yake, kama mhariri wa gazeti la “Berliner Zeitung”. Ameandika:

“Wengi wanadai Kansela Angela Merkel aseme kabisa vipi anataka kutekeleza mageuzi ya nchi hii. Lakini înafahamika kwa nini hana mamlaka ya kuongea wazi. Anajua kwamba ndani ya chama chake kuna wanasiasa wengi wenye nguvu wa kumuathiri Kansela huyu. Kwa hivyo, hotuba yake ina maana moja tu, yaani likizo imeisha.”

Mhariri wa gazeti la “Südkurier” la mjini Konstanz anajihusisha na jeshi la kimataifa la kuhakikisha amani kati ya Israel na Libanon. Ameandika:

“Kufikia makubaliano kati ya Israel na kundi la Hisbollah ya kumaliza mapigano tayari ilikuwa kazi ngumu. Kinachofuata sasa ni kukusanya wanajeshi kwa hatua ya kijeshi ya Umoja wa Mataifa ya kuhakikisha amani hiyo, lakini tena hiyo ni kazi ngumu: Uingereza haitakiwi kwa sababu ina upendeleo. Ufaransa iliahidi kupeleka idadi kubwa ya wanajeshi lakini haikutekeleza ahadi hiyo. Ujerumani inataka amani, lakini wakati huo huo, inataka wanajeshi wake wabaki kwenye meli za kijeshi, kwani katika nchi kavu hatari ni kubwa mno. Sasa Italia imepelekewa ombi la kuongoza jeshi hilo na imakubali kufanya kazi hiyo.”

Tukizungumzia amani, lazima pia kuiangalie Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ambapo pia kuna jeshi la Kimataifa la kulinda amani – hata hivyo halikuweza kuzuia mapigano, kama tunavyosoma katika gazeti la “Nürnberger Zeitung”:

“Mapigano yaliyozuka mjini Kinshasa baada na kabla ya kutangazwa matokeo ya kwanza ya uchaguzi huo, yanatia wasiwasi. Tayari wanajeshi wa Umoja wa Mataifa, MONUC, na wale wa Umoja wa Ulaya wameshindwa kuyazuia mapigano haya kati ya wafuasi wa rais Joseph Kabila na mpinzani wake Jean-Pierre Bemba. Tena wanajeshi wa Kijerumani wapo kati kati. Nini basi kitatokea wakati matokeo ya mwisho yatakapotangazwa?”

Mada nyingine inayozungumziwa ni mkutano wa mjini Stockholm kuhusu maji. Mhariri wa “Wetzlarer Neue Zeitung” ameandika hivyo kuhusu tokeo hili:

“Wataalum wanaokutana mjini Stockholm wanakabiliwa na matatizo mengi, lakini wakati huo huo wanasema kwamba uhaba wa maji unasababishwa hasa na kutokuwepo usawa katika kuyagawa maji. Kwa hivyo ni suala la kijamii. Ili kufikia lengo lao la kuhakikisha watu wote duniani wanapata maji safi, lazima wasizungumzie tu teknolojia kama pambo au namna za kusafisha maji bali pia kufikiria vipi tabaka zote za jamii zitahakikishiwa zinapata maji.”

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW