1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya kuwania Mariupol yapamba moto Ukraine

21 Machi 2022

Mapambano ya kuwania bandari ya kimkakati ya Mariupol yameendelea Jumatatu, baada ya Ukraine kukataa sharti la Urusi la kuhamisha wanajeshi wake kutoka mji huo uliozingirwa huku uvamizi wa Urusi ukiingia siku yake ya 26.

Ukraine I Mariupol
Picha: Alexey Kudenko/SNA/IMAGO

Katika mji wa bandari wa Mariupol ambao umeshuhudia mapigano makali zaidi tangu kuanza kwa uvamizi, wanajeshi wa Urusi na Ukraine wanapigana jengo kwa jengo kuwania udhibiti wa mji huo ambako watu wasiopungua 2,300 wamekufa, baadhi wakizikwa katika makaburi ya halaiki.

Vita vya Urusi nchini Ukraine, ambavyo Jumatatu vimeingia siku ya 26, havionyeshi dalili za kupungua. Uvamizi huo tayari umesababisha uharibifu na adha kubwa kwa raia. Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni 3.38 wameikimbia Ukraine.

Maafisa wa Ukraine walikataa pendekezo la Urusi kwamba wanajeshi wake waruhusiwe kutoka kwa usalama nje ya mji huo uliozingirwa, hatua ambayo ingeikabidhi Mariupol kwa Urusi, na kuruhusu vikosi vyake vilivyopo kusini na mashariki mwa Ukraine kuungana.

Rais Zelenskiy amesema haijulikani wazi ni watu wangapi wamenusurika katika shambulizi la Urusi dhidi ya shule ya Sanaa, akisema tu kwamba wapo chini ya kifusi.

Wa-Ukraine waapa kutetea maeneo yao

02:15

This browser does not support the video element.

Soma pia: Ukraine yakataa wito wa Urusi kwa Mariupol kujisalimisha

Shambulio hilo ndiyo mara ya pili katika muda wa chini ya wiki moja kulenga jengo la umma ambako wakaazi wa Mariupol wamejihifadhi.

Jumatano iliyopita, bomu lilipiga ukumbu wa sanaa ambako zaidi ya watu 1,000 waliaminika kujihifadhi, na haikuwa wazi watu wangapi waliuawa katika shambulio hilo.

Tahadhari ya vikwazo zaidi dhidi ya sekta ya mafuta ya Urusi

Huku hayo yakijiri, waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte ameutahadharisha Umoja wa Ulaya kuwa makini wakati ukiziwekea vikwazo vipya kampuni za gesi na mafuta za Urusi, kwa sababu baadhi ya mataifa ya umoja huo yanategemea pakubwa rasilimali hizo.

Akizungumza kwenye mkutano wa pamoja wa habari mjini Vilnius baada ya mazungumzo na rais wa Lithuania Gitanas Nauseda, Rutte ameonya kwamba itakuwa changamoto kubwa kwa Umoja wa Ulaya kuhakikisha uhuru wa haraka kutoka rasilimali za nishati za Urusi.

Soma pia: Marekani, washirika wazidisha shinikizo la kiuchumi kwa Urusi

"Tunapaswa kuhakikisha kwamba utegemezi wa nishati, na uhakikisho kamili kwamba utakuwa na gesi na mafuta ya kutosha katika mfumo wako pia bado ni muhimu sana kwa Uholanzi, kwa Ujerumani, kwa Ufaransa na pia kwa nchi za Ulaya Mashariki. Kwa hiyo, ndiyo, tunakubali tunahitaji kuifanya haraka iwezekanavyo, lakini hatuwezi kufanya hivi kesho," aliwaambia waandishi wa habari.

Zaidi ya wakimbizi milioni 2.8 wamekimbia vita Ukraine

01:27

This browser does not support the video element.

Urusi yazipiga marufuku Facebook na Instagram

Mahakama ya Urusi siku ya Jumatatu iliipiga marufuku mitandao ya Facebook na Instagram kwa kueneza "itikadi kali", ikiwa ni sehemu ya juhudi kubwa za Moscow kukabiliana na mitandao ya kijamii wakati wa mzozo nchini Ukraine.

Mamlaka ya Urusi imeishutumu kampuni kubwa ya kiteknolojia ya Marekani ya Meta -- kampuni mama ya Facebook, Instagram na WhatsApp -- kwa kuruhusu "chuki dhidi ya Urusi", tangu Rais Vladimir Putin atume wanajeshi Ukraine mnamo Februari 24.

Facebook na Twitter zimekuwa hazipatikani nchini Urusi tangu mapema Machi na Instagram ilizuiwa nchini wiki moja iliyopita.

Soma pia: EU yaungana kuhusu Ukraine, lakini haitatoa uanachama wa haraka

Mahakama ya wilaya ya Tverskoi ya Moscow ilikubali ombi la waendesha mashtaka la kutaka mitandao hiyo miwili ya kijamii ipigwe marufuku kwa "kutekeleza shughuli za itikadi kali".

Mahakama hiyo imeamua kuwa huduma ya Meta ya WhatsApp Messenger isingefungiwa kwa sababu haitumiwi kuchapisha taarifa za umma. Hakukuwa na tamko la mara moja kutoka kampuni ya Meta.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo Jumatatu, idara ya usalama ya Urusi FSB iliishutumu Meta kwa kufanya kazi kinyume na maslahi ya Moscow na jeshi lake wakati wa mzozo huo.

"Shughuli za shirika la Meta zinaelekezwa dhidi ya Urusi na vikosi vyake vya jeshi," mwakilishi wa FSB Igor Kovalevsky aliambia mahakama katika taarifa iliyoripotiwa na mashirika ya habari ya Urusi.

Putin na Scholz wazungumza tena kuhusu Ukraine

01:16

This browser does not support the video element.

"Tunaiomba (mahakama) ipige marufuku shughuli za Meta na kuilazimu kutekeleza uamuzi huu mara moja," alisema.

Meta ilitangaza mnamo Machi 10 kwamba majukwaa yake yangeruhusu taarifa kama "kifo kwa wavamizi wa Urusi" lakini sio vitisho vya kuaminika dhidi ya raia.

Soma pia: Mitandao ya Kijamii yalaumiwa kusambaa kwa Habari za Uongo

Lakini katika kile kilichoonekana kuwa udhibiti wa uharibifu, rais wa masuala ya kimataifa wa Meta, Nick Clegg, baadaye alisema sheria hizo legevu zitatumika tu kwa watu wanaotuma ujumbe kutoka ndani ya Ukraine.

China yahimiza majadiliano kumaliza mzozo

Mazungumzo na majadiliano yanapaswa kuwa njia ya msingi katika kushughulikia masuala ya kikanda na kimataifa, alisema Wang Wenbin, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumatatu.

Akifafanua maoni ya China kuhusu mzozo wa Ukraine, msemaji huyo alinukuu matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumapili, baada ya mazungumzo ya Wang Yi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria Ramtane Lamamra.

"Wakati Mjumbe wa baraza la taifa Wang Yi alipokutana na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, alisema hivi karibuni amebadilishana mawazo na mawaziri wengi wa mambo ya nje wa nchi za Asia na Afrika. Anahisi kuwa nchi nyingi, kama China, zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya mzozo wa Ukraine, na kushiriki maoni mengi ya kawaida.

Raia wa Ukraine waliopo Tanzania wauzungumzia mzozo wa nyumbani kwao.

01:23

This browser does not support the video element.

Soma pia: Watendaji Facebook, Twitter, Google kutoa ushahidi katika seneti

Kwanza, wote wanaamini kwamba madhumuni na kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kuzingatiwa, mizozo ya kimataifa inapaswa kutatuliwa kwa amani, na pande zinazohusika zinapaswa kutambua usitishaji mapigano na kukomesha vita haraka iwezekanavyo," Wang Wenbin alisema.

Msemaji huyo alisema mzozo wa Ukraine unaendelea kwa njia ambayo inakwenda zaidi ya yenyewe, na athari zake zikienea dunia nzima. Katika suala hili, nchi nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na China na nchi nyingine zinazoendelea, zinashiriki wasiwasi na kushikilia misimamo sawa.

China imeepuka kuikosoa Urusi kuhusiana na uvamizi wake dhidi ya Ukraine na kusisitiza kwamba itaendeleza biashara ya kawaida na taifa hilo licha ya miito inayoongezeka ya kimataifa kuitaka iikosowe Moscow.

Manusura wa Holocaust auawa katika shambulizi lam Urusi nyumbani kwake Ukraine

Boris Romantschenko, ambaye alinusurika katika kambi nne za mateso za Wanazi wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia, ameuawa na makombora ya Urusiyaliyoshambulia nyumba yake katika mji wa Kharkiv wa Ukraine, wakfu wa Kumbukumbu ya Buchenwald ulisema Jumatatu. Alikuwa na umri wa miaka 96.

"Ni kwa masikitiko kwamba tunalazimika kuripoti kifo cha vurugu cha Boris Romantschenko katika vita vya Ukraine," wakfu wa Buchenwald na Mittelbau-Dora ulisema katika taarifa.

Romantschenko alikufa nyumbani mnamo Machi 18 baada ya jengo lake kulipuliwa kwa bomu katika jiji la mashariki lililoshambuliwa sana, taarifa hiyo ilisema, ikinukuu taarifa kutoka kwa mwanawe na mjukuu wake.

Ikimuelezea kama "rafiki wa karibu", taasisi hiyo ilisema Romantschenko alijitolea kuwaelimisha wengine kuhusu maovu ya enzi ya Nazi na alikuwa makamu wa rais wa Kamati ya Kimataifa ya Buchenwald-Dora. 

Soma pia: Urusi yashambulia hospitali tatu Ukraine

Romantschenko alizaliwa katika familia ya wakulima huko Bondari, karibu na jiji la Kiukreni la Sumy, Januari 20, 1926.  

Ingawa hakuwa Myahudi, alichukuliwa na askari wa Ujerumani alipokuwa na umri wa miaka 16 na kuhamishwa mji wa Ujerumani wa Dortmund mwaka wa 1942 kufanya kazi ya kulazimishwa, kama sehemu ya mbinu za vitisho vya Wanazi dhidi ya wakazi wa Ukraine wakati huo.

Wakfu Buchenwald iumesema kifo cha Romantschenko "kinaonyesha jinsi vita vya Ukraine vilivyo hatari, pia kwa waathirika wa kambi za mateso".

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW