1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano ya Sudan yanazidi kulididimiza taifa hilo

10 Agosti 2023

Maafisa wa UN wamesema miezi 4 ya mapigano Sudan, yanazidi kuididimiza nchi hiyo pabaya huku mamilioni ya raia wakikwama katika janga la kibinaadamu na pakiwepo pia hatari ya mzozo wa kikabila kuibuka katika kanda nzima.

Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York
Mkutano wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa uliojadili mgogoro wa Sudan mjini New York Picha: Eskinder Debebe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Katika maelezo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, msaidizi wa Mkuu wa Umoja huo Martha Pobee akiwa pamoja na Mkurugenzi wa operesheni katika mashirika ya kiutu Edem Wosornu, wameielezea hali kuwa mbaya bila ya dalili zozote za kupatikana suluhu ya mzozo huo, ambao serikali mwezi Juni ilisema watu 3000 tayari wameshauwawa. Hakuna idadi yoyote ya walioangamia iliyotolewa kuanzia wakati huo.

Wosornu amesema uwezekano wa kuwepo janga la kibinaadamu ni mkubwa. Amesema watu milioni 4 wameikimbia nchi hiyo huku wengine milioni 20 ambayo ni zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu Sudan wakikabiliwa na viwango vikubwa vya usalama wa chakula au njaa.

Mapigano kati ya vikosi vilivyotiifu kwa Kiongozi wa kijeshi Sudan jenerali Abdel Fattah al Burhan dhidi ya kiongozi wa kikosi chenye nguvu cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo na yameendelea kushika kasi hasa katika mji Mkuu Khartoum na miji mingine iliyoko karibu.

OCHA: Watu milioni 3 wameyakimbia makaazi yao kutokana na vita nchini Sudan

Martha Pobee msaidizi wa Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameelezea wasiwasi wake juu ya mashambulizi dhidi ya raia pamoja na miundo mbinu, visa vingi vya unyanyasaji wa kingono pamoja na watoto kuuwawa na wengine kusajiliwa vitani.  Pobee amesema visa vya utekaji nyara na kuuwawa kwa wanaharakati wa kutetea haki za bidaamu pia vimeongezeka. Amesema kadri vita vinapoendelea ndivyo hatari ya mpasuko nchini humo inazidi kutanuka na mustakabali wa taifa zima kupotea hasa vijana.

Sudan yasema mzozo uliopo unahitaji mtazamo mpya

Kiongozi wa kijeshi Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Al-Harith Mohamed ameliambia Baraza hilo la Umoja wa Mataifa kwamba, mzozo unahitaji mtazamo mpya ili kuelewa kile kinachoendelea Sudan huku akisema kwa kuuangalia mzozo kama vita kati ya pande mbili za jeshi na wafuasi wao hakutaleta suluhu ya tatizo lililopo. Amesisitiza kuwa mzozo wa fitna unatokana na mataifa ya nje kuingilia masuala ya ndani ya Sudan.

Amnesty Inernational: Pande zinazozozana Sudan zatenda uhalifu wa kivita

Huku hayo yakiarifiwa jana Jumatano Marekani iliishutumu Sudan kutishia kuuondoa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, iwapo ujumbe huo utaliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya ukatili ndani ya mzozo unaoendelea.

Balozi Linda Thomas-Greenfield alisema walitarajia Volker perthes muakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Sudan na mkuu wa ujumbe wa UNITAMS kuzungumza katika baraza hilo lakini wanaelewa kuwa serikali ya Sudan tayari ilishatoa onyo dhidi ya mkuu huyo kutoa taarifa katika Baraza hilo huku akitahadharisha kuwa tabia hiyo haikubaliki. Sudan kwa upande wake imekanusha kutoa onyo hilo.

Chanzo: ap/afp