1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mapigano yaendelea kati ya jeshi la Sudan na RSF

Hawa Bihoga
3 Novemba 2023

Mapigano makali yameendelea huko El Geneina, mji mkuu wa jimbo la Darfur Magharibi, mwa Sudan kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF. Mapigano hayo yalizuka wakati RSF walipotaka kuteka kambi ya jeshi katika mji huo.

Moshi ukifuka hewani baada ya mashambulizi kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF
Moshi ukifuka hewani baada ya mashambulizi kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSFPicha: Ahmed Satti/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Sudan mapigano hayo yalizuka baada ya wanamgambo wa RSF walipotaka kuteka moja ya kambi za jeshi katika mji huo.

Kufuatia mapigano hayo idadi ya wananchi waliouwawa hadi sasa haijajulikana, wengine wakijeruhiwa na idadi kubwa wakiyakimbia makaazi yao.

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa jeshi la serikali limekataa pendekezo la viongozi wa kikabilala kukabidhi kambi yake ya 15 ili kubadilishana na askari na maafisa wake waondoke salama kuelekea katika mji wa Adre nchini Chad."

Mapigano hayo yamesababisha hasara kubwa katika uwanja wa mapambano ikiwemo, jeshi la Sudan kutwaa kambi za wanamgambo wa RSF katika maeneo kadhaa ya mji wa Darfur.

Soma pia:RSF wachukuwa udhibiti wa Kordofan Magharibi

Hata hivyo kiongozi wa wanamgambo wa RSF Luteni jenerali Mohamed Hamdan Dagalo hapo jana kupitia video iliosambaa katika mitandao ya kijamii aliwapongeza wanamgambo wake kwa kile alichokitaja ni mafanikio katika uwanja wa vita huko Darfur.

Aliongeza kwamba mazungumzo ya Saudi arabia kati ya kundi lake na jeshi la Sudan "lazima yafikie amani ya kweli".

UNHCR: Wakimbizi wa Sudan wanaongezeka

Wakati mapigano makali huko Darfur yakizuka kwa mara nyingine na kusababisha maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao na wengine kujeruhiwa, Shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limesema kwamba watu takriban milioni sita wamelazimishwa kuyahama makazi yao, hiyo ikiwa ni wastani wa watu milioni moja kila mwezi.

Mfanyakazi wa shirika la misaada Sudan akimsaidia mtoto na mamake yake anaekimbia mapigano Sudan Picha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Afisa wa ngazi za juu wa UNHCR Mamadou Dian Balde ameonya kwamba wakati jumuiya ya kimataifa ikijielekeza katika vita huko Gaza, idadi ya watu wanaokimbia makazi yao nchini Sudan imeanza kuongezeka tena, wakati vikosi vya RSF vikisonga mbele kuelekea katika mji wa Nyala ambao ni wa pili kwa ukubwa huko Darful.

Baadhi ya wananchi wanasema walikuwa na matumaini na mazungumzo ya Saudi Arabia yatafikia uwamuzi wa kusitishwa mapigano kwa pande zinazohasimiana, lakini matumaini yanafifi, wamepoteza makaazi, ajira na hata maisha ya wasudani wasio na hatia.

"Vita vinaendelea bila huruma." Alisema Rashid Mohamed Ahmed raia wa Sudan ambae yupo kwenye moja ya kambi za wakibizi.

"Tunaamka kila siku tukiwa na matumaini kwamba suluhu au makubaliano au usitishaji mapigano utafikiwa."

Aliongeza kwamba kwa kile kinachoendelea katika taifa lake baina ya pande zinazohasimiana, matumaini haya yanafifia siku baada ya siku.

Soma pia:Umoja wa Mataifa unavitaja vita nchini Sudan kuwa ni mzozo mbaya kabisa wa kiutu wa hivi karibuni

Jana Alhamisi Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alilionya jeshi la Sudan, dhidi ya kile Washington ilisema ni dalili za "mashambulizi makubwa yanayokaribia" katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini ambapo maelfu wamekimbia mapigano.

Marekani ambayo haikutaja chanzo cha taarifa hiyo imezitaka pande zote za mzozo kusitisha mapigano.

Tangu Aprili, vita kati ya vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na wanamgambo wa RSF, chini ya  Mohamed Hamdan Daglo, vimeua zaidi ya watu 9,000 na zaidi ya milioni 5.6 kukimbia makazi.

 Pande hizo mbili zilirejea kwenye mazungumzo wiki iliyopita mjini Jeddah yaliyosimamiwa naMarekani na Saudi Arabia, lakini maafisa wa Marekani wanasema malengo kwa sasa ni usitishaji mapigano na kuruhusu misaada ya kiutu kuingia ndani ya Sudan.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW