Mapigano yaendelea katika mji wa Syria, Aleppo
26 Julai 2012Kamanda wa kundi la waasi la Jeshi Huru la Syria Abou Omar al-Halabi ameliambia shirika la habari la dpa kwa njia ya simu kuwa wapiganaji wao sasa wanadhibiti asilimia 50 ya Aleppo. Kwamba wamezuia takribani mashambulizi mawili makuu ya wanajeshi wa serikali.
Amesema ndege za kivita zimekuwa zikifanya mashambulizi ya angani tangu afajiri katika eneo la Salahedinne na Mashaad viungani mwa Aleppo ili kuzuia kuwasili kwa wanapiganaji zaidi wa waasi.
Hujuma zaendelea mjini Damascus
Mapigano yamepamba moto mjini Aleppo tangu vikosi vya waasi vilipoanzisha mashambulizi tarehe 20 Julai ili kukidhibiti kituo hicho cha kibiashara nchini Syria, katika hatua ambayo wachambuzi wanasema inalenga kuweka ngome ndani ya nchi hiyo karibu na makao makuu ya jeshi la waasi katika upande wa mpaka nchini Uturuki.
Mjini Damascus, mapigano ya mitaani yanaendelea katika kambi ya Kipalestina ya Yarmouk kusini mwa mji huo mkuu, kulingana na kundi la kutetea haki za binadaamu la Syria.
Baada ya siki kadhaa ya mapigano katuika mji wa Damascus, wanaharakati wanasema vikosi vya serikali vimedhibiti sehemu kubwa ya mji huo, huku kukiwa na waasi wachache tu waliosalia.
Na wakati mapigano yakiendelea, maafisa wakuu katika serikali ya Bashar al Assad wanaendelea kujiondoa serikalini. Matekani jana ilidhibitisha kujiondoa serikalini kwa wanadiplomasia wawili zaidi wa Syria, ambao ni Mabalozi wan chi hiyo katika Umoja wa Falme za Kiarabu, na Cyprus, ambao ni mume na mke.
Juhudi za kidiplomasia zaendelea
Mkuu wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa Herve Ladsous, wakati huo huo amesema aliwaambia maafisa wa Syria kuwa bila kupungua kwa kiasi kikubwa machafuko, basi waangalizi waliosalia 150 wa Umoja wa Mataifa wataondoka katika siku ya mwisho ya kipindi cha siku 30 kilichorefushwa, jinsi ilibvyokubaliwa na Baraza la Usalama mnamo tarehe 20 Julai.
Wakati huo huo, katika juhudi za kurejesha mpango wa kidiplomasia, Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin amesema Urusi iko tayari kuandaa mazungumzo baina ya pande mbili zinazozozana.
Urusi imemlinda mshirika huyo wake tangu enzi za Kisovieti na wiki iliyopita, ikishirikiana na China, ilipiga kura ya turufu kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria kwa mara ya tatu hali iliyozikasirisha nchi za magharibi.
Marekani, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani zimesema zitatafuta hatua nyengine dhidi ya serikali ya Syria nje ya Baraza la Usalama. Hata hivyo nchi hizo zote zimekataa kutoa msaada wa kijeshi kwa upinzani nchini humo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman