1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Khartoum bado yatikiswa na mapigano makali

19 Mei 2023

Mashambulizi makali ya anga yameendelea kutikisa maeneo ya kusini mwa mji mkuu wa Sudan wa Khartoum huku mapigano yakipamba moto karibu na kambi ya kijeshi.

Sudan Khartoum| Moshi
Sudan, KhartoumPicha: Ahmed Satti/Anadolu Agency/picture alliance

Kwa mujibu wa mashuhuda, mashambulizi hayo ya anga ya jeshi dhidi ya wanamgambo wa Rapid Support RSF, yalisikika katika makaazi kadhaa ya vitongoji kusini mwa Khartoum, pamoja na karibu na kambi ya Taiba , huku kikosi cha akiba cha polisi kikishirikiana na jeshi kupambana na wanamgambo wa RSF.

Jeshi limekuwa likitumia zaidi mashambulizi ya anga na silaha nzito wakati likijaribu kuwarejesha nyuma wanamgambo wa RSF ambao wamesambaa viunga vya maeneo ya Khartoum na miji inayopakana ya Bahri na Omdorman.

Wakaazi wa Khartoum wakikimbia makaazi yaoPicha: AFP

Vurugu pia zimeripotiwa magharibi mwa Khartoum katika eneo la Nyala, moja ya miji mikubwa ya Sudan na mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini. Mmoja wa mashuhuda amedai kwamba milio ya silaha nzito ikiwa ni pamoja na mizinga imesikika kwa mara ya kwanza tangu makubaliano ya kusitisha mapigano. Magenge yenye silaha yameanza uporaji katika mji mwingine mkubwa wa El Obeid, ambao ni kitovu cha biashara katika jimbo la Kordofan Kaskazini.Milipuko yaendelea Sudan huku vita vikiingia mwezi wa pili

Viongozi wawili wanaowania madaraka, kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana kama Hemedti, wanadhaniwa kusalia Khartoum wakati wote wa mapigano. Siku ya Jumatano jeshi lilitoa video ikimuonyesha Burhan akiwasalimia wanajeshi katika kile kilichoonekana kuwa ni makao makuu ya jeshi katikati mwa Khartoum.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, zaidi ya watu laki 840,000 wamekimbia makaazi ndani ya Sudan na wengine zaidi ya laki 200,000 wamekimbilia nchi za jirani. Shirika la mpango wa chakula la Umoja la Mataifa limesema kuwa linazidisha operesheni zake angalau katika majimbo sita ya Sudan ili kuwasaidia watu takriabni milioni 5 walio hatarini na kuwasaidia wengine wanaokimbilia nchi za Chad, Misri na Sudan Kusini.Mapigano makali yaendelea nchini Sudan

Maafisa wa Sudan na wawakilishi wa UN juu ya mzozo wa misaada ya kiutuPicha: REUTERS

Umoja wa Mataifa kupitia afisa anayehusika na misaada ya kiutu Martin Griffiths, umelaani ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya pande zinazozozana nchini humo wiki iliyopita na kutoa rai ya kuruhusu misaada inayohitajika kwa haraka. Griffiths ambaye anaongoza juhudi za kiutu za Umoja wa Mataifa, alikaribisha makubaliano ya Mei 12 yaliyotiwa saini mjini Jeddah na pande mbili katika mzozo huo zilizoapa kujizuia kushambulia misafara ya misaada.

"Kutiwa saini kwa hati hiyo, pamoja na ulinzi wake wa matakwa ya kibinadamu, inasisitiza kwamba hakupaswi kuwepo na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu au majengo. Siku mbili zilizopita kulikuwa na shambulio kwenye ofisi ya Mpango wa Chakula Duniani huko Khartoum, kwa mfano na kumekuwepo na mengine"

Umoja wa Mataifa ulisema kuwa nusu ya wakazi wa Sudan wanahitaji msaada wa kibinadamu, na kwamba zaidi ya dola bilioni 3 zitahitajika mwaka huu pekee kutoa msaada wa haraka ndani ya nchi hiyo na kwa wale wanaokimbia kuvuka mipaka yake. Hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 1,000, na takriban wengine milioni 1 kuyahama makazi yao na kuwaacha wakaazi wa Khartoum wakihangaika kujinusuru.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW