Mapigano yaendelea Kongo licha ya makubaliano
22 Oktoba 2025
Katika jimbo la Kivu Kaskazini, mapigano mapya yameripotiwa tangu Jumatatu kati ya AFC/M23 na makundi ya Wazalendo katika vijiji vya Nyabiondo na Kaanja, eneo la Masisi. Jana Jumanne, mapigano mengine makali yalitokea katika vijiji vya Kinyana na Bibwe, eneo la Bashali Mokoto wilayani Masisi.
Kwa upande wa Kivu Kusini hali ya taharuki imeripotiwa katika vijiji vinavyopakana na mbuga ya wanyama ya Kahuzi-Biega wilayani Kabare, na katika maeneo ya Walungu ikiwemo Nyangezi, Mazigiro, Lurhala na Kamisimbi, ambako mapambano makali kati ya AFC/M23 na Wazalendo yameripotiwa katika vijiji vya Kahinga, Itara, Chishendo, Chamasiga, Lwana na Bushigi.
Mick Mutiki, mtaalamu wa masuala ya usalama Mashariki mwa Kongo anasema mgawanyiko na ukosefu wa uratibu miongoni mwa makundi ya Wazalendo ndio chanzo kikuu cha mvutano hali ambayo inaweza kuhatarisha utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano:
Katika taarifa yake ya hivi karibuni, AFC/M23 imeishutumu serikali ya Kinshasa kwa kuchochea mapigano na kuwatisha raia katika maeneo iliyo nayo chini ya udhibiti.
Jeshi ladaiwa kufanya mashambulizi ya makusudi ya droni
Msemaji wa kundi hilo, Lawrence Kanyuka amedai kuwa jeshi la serikali lilifanya mashambulizi ya makusudi kwa kutumia ndege zisizo na rubani katika maeneo yenye wakazi wengi ya Nyarushyamba (Masisi) na Kashebere (Walikale), akisema huo ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji mapigano. Amesema AFC/M23 itaendelea kujilinda na kulinda raia wake dhidi ya tishio lolote.
Hata hivyo, Jeshi la Kongo (FARDC) limekanusha tuhuma hizo na badala yake limeituhumu AFC/M23 kwa kuvunja makubaliano hayo. FARDC pia imepinga taarifa za kuhamisha wanajeshi na vifaa kutoka Bujumbura, likisema huo ni upotoshaji. Msemaji wa jeshi hilo mkoani Kivu Kusini, Luteni Mbuyi Kalonji Reagan, amesema jeshi liko tayari kujibu uvunjifu wowote wa usitishaji mapigano.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Mkuu anaehusika na Ulinzi wa Kitaifa na Wapiganaji, Guy Kabombo Muadiamvita, yuko Brazil kwa ziara rasmi katika jiji la São Paulo, akijifunza kuhusu uboreshaji wa teknolojia ya kijeshi na anatarajiwa kukutana na Waziri wa Ulinzi wa Brazil, José Múcio Monteiro kwa ajili ya kutia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi kati ya nchi hizo mbili.