1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea kurindima Tripoli

28 Mei 2019

Mapigano makali yamekuwa yakikaribia katikati ya mji mkuu wa Libya, Tripoli, huku wanajeshi watiifu kwa kamanda wa Libya Khalifa Haftar wakipambana kuchukua madaraka

Krieg in Libyen
Picha: Getty Images/M. Turkia

Hiftar alianzisha mashambulizi ya kijeshi mjini Tripoli mapema mwezi wa Aprili, licha ya ahadi za kuelekea katika uchaguzi katika taifa hilo la Afrika Kaskazini.

Libya imegawika kati ya Hiftar, ambaye jeshi lake linalojiita Libyan National Army linadhibiti mashariki na sehemu kubwa ya kusini, na Waziri Mkuu wa Libya Fayez Sarraj, ambaye anaiendesha serikali inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli ambayo ni dhaifu.

Katika wiki za karibuni, makabiliano yalikuwa yamepungua kutokana na kuanza kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Lakini katika siku chache zilizopita, mzingiro wa mji mkuu ukaanza tena kwa kushuhudia mashambulizi makali. Wanajeshi wa Haftar wameendeleza kampeni yao katika viiunga vya mashariki na kusini mwa Tripoli.

Wanajeshi wa Fayez na Khaftar wana wanawania udhibiti wa TripoliPicha: picture-alliance/C. Liewig

Ofisi ya habari za LNA imesema wamechukua udhibiti wa maeneo yaliyo karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tripoli, ambao uliharibiwa kwa kiasi kikubwa katika vita vya wenywe kwa wenyewe kufuatia kuangushwa kwa aliyekuwa dikteta wa muda mrefu Muammar Gaddafi mwaka wa 2011.

Saraj al-Majbri, msaidizi wa mkuu wa majeshi wa LNA amesema wanajeshi wake pia wameingia katika eneo la Salah al-Deen, kilomita chache kutoka katikati ya mji mkuu. Amedai kuwa harakati za wanajeshi wake kuelekea katikati ya mji zilipunguzwa katika wiki chache zilizopita kwa sababu hawakutaka kutumia silaha nzito katika maeneo ya wakaazi wengi.

Hiftar amesema hatositisha mashambulizi yake ili mradi makundi ya wapiganaji yataendelea kudhibiti Tripoli, na akadai kuwa wapiganaji hao wanaendelea kudhibiti makao makuu ya serikali ya Waziri Mkuu Fayez Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Duru sita za mazungumzo na serikali yameshindwa kufikia makubaliano ya kisiasa.

Umoja wa Mataifa umesema jana kuwa mapigano yamesababisha vifo vya karibu watu 562, wakiwemo raia 40. Iliongeza kuwa miongoni mwa waliouawa, ni wafanyakazi wawili wa afya, wakati makombora yalipoyapiga magari ya kuwasafirisha wagonjwa kusini mwa Tripoli Alhamisi wiki iliyopita