1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan

Mapigano yaendelea kushuhudiwa nchini Sudan

5 Juni 2023

Mapigano makali yameendelea kushuhudiwa sehemu mbalimbali nchini Sudan baada ya muda wa usitishwaji mapigano kufikia tamati wikiendi hii. Ghasia zimeshuhudiwa katika mji mkuu Khartoum, huku watu 40 wakiuawa huko Darfur.

Sudan | Kämpfe in Khartum
Picha: Mohamed Nureldin Abdallah/REUTERS

Muda uliopangwa wa makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani na Saudi Arabia ulifikia tamati siku ya Jumamosi jioni. Hilo limepelekea kuzuka tena kwa mapigano huko Khartoum na kwengineko na kusababisha uharibifu mkubwa, vitendo vya uporaji, kuathirika kwa huduma za afya, kukatika kwa umeme na maji, na kupungua kwa usambazaji wa chakula.

Maeneo kulikoripotiwa mapigano ni kusini na katikati mwa jiji la Khartoum,  mji wa Bahri na kaskazini mwa mji wa Blue Nile. Wanaharakati wamesema pia kuwa ghasia zilizuka katika jimbo la Magharibu mwa Sudan la Darfur na kusababisha vifo vya watu wapatao 40 na wengine kadhaa kujeruhiwa wakiwemo wakazi wa kambi ya Kassab.

Mashuhuda wameripoti kuwa ndege ya kivita ilianguka huko Omdurman, moja ya miji mitatu inayozunguuka mto Nile na uliyo miongoni mwa miji inayounda mji mkuu. Jeshi halikuzungumzia chochote juu ya tukio hilo, licha ya kuwa imekuwa ikitumia mara kadhaa ndege za kivita ili kulenga ngome za vikosi vya RSF.

Mvua zasababisha hofu Sudan

Raia wa Sudan wakishuhudia uharibifu mkubwa kutokana na mvua kubwa Agosti 13,2022Picha: Sami Alopap/AA/picture alliance

Katika siku za hivi karibuni mvua zimeanza kunyesha na kuashiria mwanzo wa msimu wa mvua utakaoendelea hadi mwezi Oktoba na kusababisha mafuriko na hatari ya kutokea kwa miripuko ya magonjwa.

Mvua hizo zinaweza kutatiza juhudi za utoaji msaada ambazo tayari zimechelewehwa kutokana na urasimu na changamoto za upatikanaji wa vifaa. Wafanyakazi wa misaada wameonya kuwa maiti zimeachwa mitaani huku takataka ambazo hazijakusanywa zimekuwa zikirundikana.

Soma pia: Miili 180 yazikwa bila ya kutambuliwa kufuatia mapigano makali Sudan

Saudi Arabia na Marekani zimesema zinaendelea na mazungumzo ya kila siku na wajumbe kutoka pande mbili hasimu, ambao wamesalia mjini Jeddah ingawa mazungumzo ya kuongeza muda usitishaji mapigano yalisitishwa wiki iliyopita.

Riyadh na Washington wamesema majadiliano hayo yanalenga kuwezesha utoaji wa misaada ya kibinadamu na kufikia makubaliano juu ya hatua za muda mfupi zinazotakiwa kuchukuliwa na pande mbili hasimu kabla ya kuanza tena kwa mazungumzo mjini Jeddah.

Majenarali wawili hasimu nchini Sudan. Kulia: Mohamed Hamdan Dagalo na kushoto: Abdel Fattah al burhanPicha: Bandar Algaloud/Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo, ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kuwa alizungumza kwa njia ya simu na Waziri wa mambo ya nje wa Saudia na kujadili kuhusu juhudi za upatanishi kunako makubaliano ya Jeddah.

Dagalo anayefahamika zaidi kama Hemedti haijulikani aliko kwa sasa ingawa alionekana kwenye picha za video akiwa na wanajeshi wake katikati mwa jiji la Khartoum mwanzoni mwa mzozo huo wa madaraka kati ya majenerali wawili hasimu ulioanza Aprili 15 mwaka huu na kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu ambapo zaidi ya watu 1, 800 wameuawa, wengine milioni 1.2 wamekuwa wakimbizi wa ndani na 400,000 wakikimbilia nchi jirani.

Soma pia: Mapigano yaendelea Sudan licha ya Marekani kuziwekea pande hasimu vikwazo

Takriban watu milioni 25 ikiwa ni zaidi ya nusu ya wakazi wa Sudan sasa wanahitaji ulinzi na misaada ya kibinaadamu katika nchi ambayo kulingana na Umoja wa Mataifa ilikuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW