Mapigano yaendelea Syria
25 Septemba 2012Waziri mkuu wa Qatar Sheikh Hamad bin Jassim al Thani akitoa hoja hiyo ya kuitaka Jumuiya ya Kimataifa iingilie kati mzozo wa Syria amesema anaamini kwamba nchi za Kiarabu pamoja na nchi za Ulaya zitakuwa tayari kushiriki licha ya kujionesha hadharani kwamba haziko tayari kutuma wanajeshi katika hatua hiyo.
Waziri mkuu wa Qatar Sheikh Hamad akizungumza saa chache kabla ya hotuba ya rais wa Marekani Barack Obama katika mkutano wa kilele wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa ameitilia mkazo marekani kujihusisha zaidi katika suala la Syria akisema anataraji kwamba Washington itajishughulisha zaidi katika mzozo huo baada ya uchaguzi wa rais utakaofanyika ndani ya kipindi cha wiki sita zijazo.
Ndani ya Syria kwenyewe kwahivi sasa mapigano bado yanaendelea. Mtoto mmoja wa miaka 6 amepigwa risasi na kuuwawa na wanajeshi waliolilenga gari alilokuwemo.Mtoto mwingine amejeruhiwa vibaya katika tukio la mashambulio ya mabomu kwenye mji wa Aleppo. Pia shirika la Kimataifa la msaada kwa ajili ya watoto la Save the Children limesema kwamba watoto nchini humo wamepata kiwewe kutokana na kushuhudia mauaji na mateso pamoja na madhila mengine
.Ripoti hiyo inatolewa ikiwa ni baada ya kiasi ya watoto 12 kuwa miongoni mwa watu 116 kuuwawa kote nchini humo. Aidha waasi wanasemekana wamekimbilia katika maeneo ya milimani katika mji wa Al Atarib huko Allepo wakilenga kuishambulia kambi ya kijeshi nambari 46.Wapiganaji hao wanasema wameshaizingira kambi hiyo muhimu ya wanajeshi wa serikali na wamekuwa wakivishambulia vikosi vya Assad villivyonasa kwenye kambi hiyo katika kipindi cha siku tatu zilizopita.
Kwa mujibu wa taarifa za waasi nchini Syria kuna wanajeshi 1000 wa Assad ndani ya kambi nambari 46 ambayo ni muhimu wa jeshi la Assad ikiwa ni kiunganisho cha mwisho kwenye barabara ya kwenda mjini Allepo na wanapanga kuiripua kabisa ndani ya siku kadhaa zijazo.
Kiongozi wa waasi walioko kwenye eneo hilo Abu Sadeq amesema wanajeshi hao wamejihami wakiwa na vifaru 13 na mizinga kadhaa lakini idadi yao ni ndogo ikilinganishwa na waasi waliowazunguka na kwahivyo itakuwa vigumu wao kujinasua kutoka kwenye kambi hiyo na kwamba trayari waasi wamekaa tayari kwa magurunedi kuvizia pindi wakitoka kuwamaliza. Wakati huohuo baraza la mawaziri nchini Iraq limeamu kutoa msaada wa kiutu kwa ajili ya wasyria kupitia shirika lake la hilali nyekundu
Mwandishi:Saumu Yusuf
Mhariri :Mohammed AbdulRahman