Mapigano yaibuka kati ya kundi la wazalendo na FARDC
24 Novemba 2025
Vyanzo vya hospitali ya Uvira vimethibitisha vifo hivyo, kikiwemo cha mtoto aliyepigwa risasi wakati wa mapambano hayo. Kwa mujibu wa asasi za kiraia, tukio hilo lilianza kufuatia machafuko yaliyochochewa na Wazalendo katika uwanja wa Parokia ya Mtakatifu Paulo katika kitongoji cha Songo mjini Uvira.
Asasi hizo zinasema wapiganaji hawa walijaribu kudai sehemu ya misaada ya kibinaadamu iliyokuwa ikigawiwa kwa watu walio hatarini. Hali hiyo ilisababisha mvutano kati ya Wazalendo na askari wa Kongo waliopinga ombi la Wazalendo.
Hali imerejea kuwa shwari lakini bado wakaazi wanaishi kwa hofu
Pacifique Karauka, mwanaharakati wa shirika la raia katika Nyanda za Uvira anasema kwamba hali imerudi kuwa shwari ila hadi sasa wakaazi wa mji huo na vijiji vyake wanaishi kwa wasiwasi.
Katika upande wa AFC/M23, watu wasiopungua watano waliuawa usiku wa kuamkia leo katika maeneo mbalimbali ya kijiji cha Katana. Mashuhuda wanalinyooshea kidole kundi la M23 wakisema wapiganaji wake walifika ndani ya kituo cha afya na kupeleka wagonjwa na walinzi wao, na baadaye asubuhi miili ya mgonjwa mmoja na walinzi wawili ilikutwa kijijini, wote wakiwa ni vijana, na kwamba vijana wengi wakishukiwa tu kuwa Wazalendo wanauawa.
Kwa sasa wanaharakati wengi wa asasi za kiraia wanaishi kwa woga katika kijiji cha Katana na pia wilayani Kabare, wakisema wanaogopa kusikika sauti zao kwa sababu wanawindwa na makundi ya wapiganaji.