Mapigano yamezuka tena mashariki mwa Kongo
21 Julai 2025
Katika eneo la Uvira na Rurambo, vurugu zinaendelea, zikisababisha hofu na mashaka miongoni mwa raia waliokuwa na matumaini ya kuona amani ikianza kurejea.
Haukupita hata muda wa saa 48 baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo ya kanuni huko Doha, milio ya risasi ikaanza tena Rurambo, katika eneo la kivu kusini.
Makubaliano hayo yalitiwa saini tarehe 19 Julai kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa AFC/M23, kwa upatanishi wa Emir wa Qatar, Tamim ben Hamad Al Thani, yakiahidi kusitishwa mapigano na pande zote.
Lakini hali halisi Mashariki mwa Kongo ni tofauti kabisa. Raia wanaogopa kuona damu ikiendelea kumwagika.
"Tulisikitika sana kuona vita ikiendelea. Wakati wa vita, watu wengi hufa, na hilo si jambo jema. Ni wananchi wanaoumia. Viongozi wanapaswa kuangalia namna ya kukaa pamoja na kuelewana. Tumechoka na vita.” Mmoja wa raia alimwambia DW.
Baadhi ya raia wamesema wanapata mashaka na mkataba huo ikiwa utaleta tija ya utulivu katika eneo hilo la mashariki ambalo limekubwa na mzozo kwa zaidi ya miongo miwili.
"Hatujui kama viongozi wanafuatilia hili kwa makini. Maswali ni mengi vichwani mwetu.''
Wachambuzi: Kuna hujuma kwenye mkataba
Wakati mapigano yakiendelea huko Rurambo, umbali mfupi kutoka Uvira, Philémon Ruzinge, mchambuzi kutoka Goma, anaamini kuwa kuna hujuma dhidi ya mikataba yote inayotiwa saini.
Kwani haiwezekani kutiwa saini makubaliano, halafu yatendwe mambo kinyume chake. Alisema:
"Kila mara kunapokuwa na makubaliano au mikutano, huwa kunafuata mashambulizi au kuchukuliwa kwa miji na wilaya. Na hii inawafanya wananchi wakose kabisa imani kwa viongozi. Kuna vurugu kati ya M23 na serikali ya Kongo. Hii ni hali ya kusikitisha sana. Hebu fikiria, haijapita hata siku tatu tangu mkataba utie saini, na tayari jana mapigano yamezuka huko Rurambo.”
Tangu mwisho wa Januari, waasi wa M23 wamepanua udhibiti wao, wakianza na Goma, kisha wakachukua Bukavu.
Na wakati wajumbe wakisaini makubaliano huko Doha, wanajeshi tayari walikuwa wakipigana milimani mwa Kivu kusini.
Makubaliano yaliyotiwa saini huko Doha hayataji moja kwa moja suala la M23 kuondoka maeneo wanayoyashikilia, kama walivyosisitiza wasemaji wao, Lawrence Kanyuka na Bertrand Bisimwa, kupitia mitandao ya kijamii.
Hivyo basi, kwa sasa, ni tamko la nia tu, linalotangulia mazungumzo rasmi yanayotarajiwa kufanyika tarehe 17 Agosti.