1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel-Hamas: 'Hakuna mahala salama Gaza,' Guterres aonya

7 Desemba 2023

Vikosi vya Israel vilikuwa vimeyazunguka makazi ya kiongozi wa Hamas Yehya Sinwar, yaliyoko katika Ukanda wa Gaza. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliarifu hayo kwenye hotuba yake kupitia televisheni.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika picha alipohudhuria mkutano na waandishi wa habari sanjari na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron Oktoba 24, 2023Picha: Christophe Ena via REUTERS

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hata hivyo alikiri kwamba yeye na wanajeshi wake hawakuwa na uhakika kama Sinwar alikuwemo nyumbani kwake.

Taarifa zimesema nyumba ya Sinwar huenda ilikuwa katika jiji la Khan Younis, ambalo ni kubwa zaidi kusini mwa Gaza, mahali ambako jeshi la Israel lilifanya mashambulizi jana Jumatano, ikiwa ni sehemu ya harakati zake za hivi karibuni kuingia katikati mwa jiji hilo.

Israel inaamini kwamba baadhi ya viongozi wa Hamas, huenda wakawa  wamejificha katika eneo hilo la kusini ama kwenye mahandaki yaliyotapakaa kwenye eneo kubwa la Gaza, baada ya wiki za kwanza za mapigano kujikita katika eneo la kaskazini mwa Gaza. Ujerumani, Umoja wa Ulaya, Marekani, Israel yenyewe na mataifa mengine yanaliorodhesha kundi la Hamas kuwa ni la kigaidi

Jeshi la Israel limesema limezingira makazi ya kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar aliyewahi kuzuiwa gerezani huko Israel kwa miaka 20Picha: Mohammed Abed/AFP

Sinwar alikuwa akizuiwa gerezani nchini Israel kwa zaidi ya miaka 20, baada ya mwaka 1988 kukutwa na hatia ya mauaji ya Wapalestina wanne na wanajeshi wawili wa Israel.

Soma pia:Netanyahu na vita mbili zinazomkabili - Hamas na nyumbani

Katika hatua nyingine wakuu wa kundi la mataifa yaliyoinukia kiuchumi ulimwenguni, G7 jana Jumatano walijadiliana juu ya mzozo huu katika kikao chao kwa njia ya video na kutoa wito wa "hatua za haraka" za kupunguza hali inayozidi kuzorota kwa raia walioko Ukanda wa Gaza.

Viongozi hao kwa pamoja wamesema wanaunga mkono na kuhamasisha usitishwaji zaidi wa mapigano ili kuruhusu misaada ya kiutu kuingia Gaza. Aidha wameitaka Iran kuacha kulisaidia kundi la Hezbollah lililoko Lebanon ama wanamgambo wa Wahouthi walioko kwenye ukanda huo, ili kuepusha uwezekano wa kusambaa kwa mapigano.

Viongozi hao aidha wamesema, ingawa waliyakaribisha makubaliano ya karibuni ya kusitisha mapigano na yaliyomalizika wiki iliyopita, bado wanasema wamesikitishwa mno na hatua ya Hamas ya kukataa kuwaachia mateka wote wa kike hali iliyosababisha mapigano kuanza upya.

Umoja wa Mataifa wachukua hatua ya nadra kuonya juu ya hali tete huko Gaza

Huku hayo yakiendelea, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye ametoa ombi la moja kwa moja kwa Baraza la Usalama juu ya hali mbaya ya kibinaadamu katika Ukanda wa Gaza, hii ikiwa ni hatua ya nadra ya kutumia kifungu hicho cha Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametumia kifungu kinachotumika kwa nadra kulitolea mwito Baraza la Usalama kuangazia hali katika Ukanda wa GazaPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Ameonya juu ya kuzorota kwa haraka hali ya kibinaadamu na pengine kuwa janga litakalowaathiri pakubwa Wapalestina pamoja na amani na usalama wa kikanda na kusema matokeo kama hayo yanatakiwa kuepukwa kwa gharama yoyote.

Soma pia:Guterres asikitishwa na kuanza upya kwa vita Ukanda wa Gaza

Guterres ametumia kifungu hicho cha 99 kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani mwaka 2017. Kifungu hicho kinasema Katibu Mkuu anaweza kuwasilisha mbele ya Baraza la Usalama suala lolote, ambalo kwa maoni yake anadhani linaweza kutishia maboresho ya amani na usalama.

Aliangazia zaidi ugumu wa kufikishwa kwa misaada ya kiutu na upatikanaji wa huduma za afya kwa watu waliozingirwa na kuhimiza usitishwaji wa mapigano.

Soma pia:Usitishwaji mapigano kuanza Gaza, mateka kuachiwa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa hivi sasa linaongozwa na Ecuador na limekwishafanya vikao kadhaa kuhusiana na mzozo huo. Hata hivyo, limekuwa likikabiliwa na migawanyiko na hasa kutokana na misimamo tofauti linapokuja suala kati ya Israel na Palestina.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW