1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yapamba moto Syria kuelekea usitishaji

11 Septemba 2016

Saa chache baada ya Marekani na Urusi kutangaza makubaliano ya kumaliza mgogoro wa kivita uliyodumu kwa miaka mitano nchini Syria, mapigano yemepamba moto upya. Karibu raia 100 wameuawa katika mashambulizi ya angani.

Syrien Aleppo Luftangriff Trümmer
Picha: picture-alliance/AA/A. Hasan Ubeyd

Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake mjini London,Uingereza, limeripoti siku ya Jumamosi kwamba raia wasiopungua 58 wameuawa katika mkoa unaodhibitiwa na waasi wa Idlib baada ya ndege za kivita kuliripua kwa mabomu soko kaskazini-magahribi mwa mji huo, saa kadhaa baada ya kutangazwa kwa masharti ya makubaliano ya kusitishwa mapigano nchini kote.

Mjini Aleppo, jeshi la Syria lilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na waasi katika jitihada za kuimarisha nafasi yake kuelekea usitishaji wa uhasama, unaoanza siku ya Jumatatu wakati wa siku kuu ya Eid al-Adha. "Mapigano yamepamba moto katika maeneo yote ya Aleppo," alisema kapteni Abdul Salam Abdul Razak, msemaji wa kundi la waasi la Brigedi za Nour al-Dine al Zinki , ambalo ni sehemu ya jeshi Huru la Syria (FSA). Watu wasiopungua 30 wameuawa katika mashambulizi hayo, kulingana na shirika la uangalizi wa haki za binaadamu.

Makubaliano kati ya Marekani na Urusi

Ongezeko hilo la machafuko linafuatia tangazo lililotolewa mapema Jumamosi juu ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Urusi baada ya mazungumzo marefu mjini Geneva, Uswisi. Chini ya makubaliano hayo. Moscow itaushinikiza utawala wa Assad kukomesha kampeni yake ya kijeshi dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Marekani.

Mawaziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry, na wa Urusi Sergei Lavrov wakitangaza makubaliano ya kusitisha mapigano Syria.Picha: picture-alliance/dpa/A.Shcherbak

Kwa Urusi kufanya hivyo, Marekani itaanzisha mashambulizi ya pamoja na Urusi dhidi ya kundi lililobadili jina la Jabhat Fatah al-Sham, zamani likijulikana kama Jabhatu Nusra wakati likiwa na mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, ikiwa makubaliano hayo yataheshiwa kwa muda usiyopungua siku saba.

"Hili linahitaji kusitisha mashambulizi, yakiwemo ya angani, na majaribio yoyote ya kutwaa ardhi zaidi kwa gharama ya pande zilizomo kwenye makubaliano ya usitishaji uhama. Inahitaji ufikishaji wa misaada usiyo na vikwazo vyovyote katika maeneo yote yaliozingirwa, ikiwemo Aleppo," alisema waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Uidhinishwaji usiyo rasmi kutoka serikali ya Syria

Serikali ya rais Bashar al-Assad haijatoa tamko rasmi kuhusu makubaliano hayo. Badala yake, shirika la habari la serikali SANA limesema serikali inayakubali mapatano hayo, na kuongeza kuwa uhasama utaanza kusita katika mji wa kaskazini wa Aleppo kwa sababu za kibinaadamu. Halikusema ni lini vurugu zitamalizika, na kuongeza kuwa makubaliano hayo kati ya Marekani na Urusi yalifikiwa kwa idhini na taarifa ya serikali.

Basma Kodmani, kutoka muungano wa upinzani unaoungwa mkono na Saudi Arabia wa Kamati Kuu ya Majadiliano (HNC) alisema kundi linachukuwa tahadhari kwa makubaliano hayo, na kuongeza kuwa kunahitaji kuwepo na mifumo ya kuhakikisha utekelezaji wake.

Vurugu za Jumamosi zinaonyesha kuwa huenda ikawa vigumu kuyatekeleza makubaliano kati ya Marekani na Urusi kwa sabau mataifa hayo mawili yana ushawishi wenye mipaka kwa serikali na makundi ya waasi kuhusu kusitisha mashambulizi.

Makubaliano ya kusitisha uhasama yaliofikiwa na mataifa hayo mawili makubwa duniani mapema mwaka huu na kuanza kutekelezwa mwishoni mwa mwezi Februari yalishindwa muda mfupi baadae na yalifuatiwa na miezi miwili ya vurugu zilizouwa maelfu.

Waokozi wakitafuta maiti na manusura katika vifusi baada ya shambulizi la angani mkoani Idlib siku ya Jumamosi.Picha: picture-alliance/AA/O. Haj Kadour

Muungaji mkono mkuu wa Assad

Urusi ndiyo muungaji mkono mkuu wa utawala wa Assad huku Marekani ikiyaunga mkono makundi ya waasi wanaotaka kum'ngoa madarakani. Vita vya Syria vilivyoigia mwaka wake wa tano, vimeendelea licha ya duru kadhaa za mazungumzo ya amani na majaribio ya jumuiya ya kimataifa kukomesha vurugu nchini humo. Watu wasiopungua robo milioni wameuwawa,na nusu ya wakaazi wa nchi hiyo kabla ya vita wamekoseshwa makaazi.

Mashambulizi ya angani ya Jumamosi yalifanyika hasa katika miji ya Aleppo na Idlib. Aleppo imekuwa kituo cha vurugu nchini Syria katika miezi ya karibuni, ambapo watu karibu 2,200 wakiwemo raia 700 wameuwawa tangu mwezi Julai mwaka huu kwa mujibu wa shirika la uangalizi w ahaki za binaadamu, linalofuatilia vurugu hizon kupitia mtandao wa wanaharakati walioko ndani ya Syria.

Mgogoro wa Syria ulianza mnamo mwaka 2011, wakativikosi vya serikali vilipoanzisha ukandamizaji wa vurugu dhidi ya waandamanaji waliokuwa wanadai demokrasia, wakimtolea mwito Assad kuachia ngazi. Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 250,000 wameuawa, na zaidi ya nusu ya wakaazi jumla wamekosa makaazi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga

Mhariri: Isaac Gamba

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW