1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaripotiwa nchini Ethiopia licha ya wito wa amani

Sylvia Mwehozi
30 Agosti 2022

Kumeripotiwa mapigano mapya katika eneo tete la Kaskazini mwa Ethiopia jana Jumatatu licha ya jumuiya ya kimataifa kutoa wito wa kusitisha machafuko mapya baina ya vikosi vya serikali na waasi wa Tigray.

Tigray-Krise in Äthiopien
Picha: Ben Curtis/AP/dpa/picture alliance

Mapigano hayo yametokea katika eneo la karibu na mji wa Kobo ulioko mkoa wa Amhara, kusini tu mwa Tigray. Pande mbili zinazozozana nchini Ethiopia, zimeshutumiana kwa kuanzisha mashambulizi Jumatano iliyopita, ambayo yamedhoofisha makubaliano ya miezi mitano ya usitishaji mapigano na kuondoa matumaini ya upatikanaji wa amani, katika taifa hilo la pili kwa idadi kubwa ya watu barani afrika.Guterres azitaka Ethiopia na Tigray kusitisha mapigano mapya

Raia mmoja wa mjini Kobo, amelieleza shirika la habari la AFP kwamba amesikia milio ya silaha nzito kuanzia majira ya asubuhi, akieleza pia kwamba watu wengi walikuwa wakimiminika kutoka maeneo ya jirani kwenda mjini, wengine wakilala kwenye varanda, huku mamlaka ikiruhusu baadhi ya waliopoteza makazi kuhifadhiwa katika mabweni ya vyuo vikuu. "Kwa sasa kuna hali ya sintofahamu huko Woldiya ingawa ni shwari kidogo kuliko jana," alisema mkazi huyo na kuongeza kuwa mji huo kwa sasa uko chini ya amri ya kutotoka nje jioni hadi alfajiri.

Serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed, ilitangaza Jumamosi kwamba imeviondoa vikosi vyake katika mji wa Kobo ili kuepusha "maafa makubwa" huku chama cha ukombozi wa watu wa Tigray TPLF ambacho kimekuwa kikipambana na vikosi vya serikali na washirika wake kwa karibu miezi 22, kikidai kuidhibiti miji mingi katika mashambulizi makubwa. Watu wanne wakiwemo watoto wawili waliuawa katika shambulio la anga ambalo liliulenga mji mkuu wa Tigray wa Mekelle siku ya Ijumaa.

Gari lililobeba vyakula vya msaada vya Umoja wa MataifaPicha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Jumuiya ya kimataifa imeelezea hali ya wasiwasi mkubwa kuhusu kuzuka upya kwa mapigano katika mzozo ambao tayari umegharimu maisha ya idadi ya raia isiyojulikana na kusababisha mzozo mbaya wa kibinadaamu. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema hali ya kibinadamu kaskazini mwa Ethiopia inaendelea kuwa ya kutisha, huku kukiwa na  ripoti ambazo hazijathibitishwa juu ya watu kuyakimbia makazi yao katika maeneo ya makabiliano kwenye mikoa ya Amhara na Afar.

Dujarric amewaeleza waandishi wa habari kwamba "usambazaji wa vifaa vya kibinadaamu kwa njia ya barabara hadi Tigray umesimamishwa tangu wiki iliyopita tarehe 24 Agosti. Vile vile, Shirika la Umoja wa Mataifa la huduma za anga la kibinadamu, halijaweza kuruka ndani na kutoka Tigray tangu agosti 25, na kusimamisha usafirishaji wa pesa taslimu pamoja na mzunguko wa wafanyikazi wa misaada."

Tume ya kimataifa ya wataalamu wa haki za binadamu iliyoteuliwa na Umoja wa Mataifa kuhusu Ethiopia, imesema kuwa "imekasirishwa" kuhusu kuibuka upya kwa mapigano na kutoa wito kwa pande zote mbili kusitisha machafuko na kurejea kwenye mazungumzo pamoja na kuyawezesha mashirika ya kibinadamu kusambaza misaada huko Tigray.

Ethiopia yailaumu TPLF kwa kutoshirikiana kutafuta amaniWito kama huo pia umetolewa na tume ya haki za binadamu ya Ethiopia, ambayo imesema "idadi ya raia katika maeneo yaliyoathirika bado wanaendelea kuteseka kutokana na kiwewe, kupoteza wapendwa wao na riziki.

Makubaliano ya usitishaji mapigano yalifikiwa mwezi Machi na kuruhusu usambazaji wa misaada ya kiutu jimboni Tigray, ambako Umoja wa Mataifa unasema mamilioni wako katika ukingo wa baa la njaa huku kukiwa na uhaba mkubwa wa fedha, mafuta na madawa.

Tangu mwishoni mwa mwezi Juni, serikali ya Abiy na waasi walielezea utayari wao wa kufanya mazungumzo ya amani lakini walitofautiana juu ya masharti ya mazungumzo hayo.