Mapigano yashika kasi Yemen
19 Oktoba 2016Kabla ya machafuko hayo mapya, serikali ya nchi hiyo ilikuwa imekubali mpango huo uliolenga kuruhusu misaada ya kibanaadamu kufika maeneo ambayo hayajafikiwa na misaada hiyo kwa miezi kadhaa.
Duru za wakazi wa mji mkuu Sanaa zimeeleza kuwa kuongezeka kwa mapigano nchini Yemen, imetolewa wakati ambapo muungano wa majeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, uliposhambulia kwa bomu kambi ya waasi katika mji mkuu. Kumesikika vishindo vikubwa vya mabomu, baada ya mashambulizi mawili ya anga yaliyofanywa na ndege za muungano huo dhidi ya eneo la waasi lililopo Mashariki mwa mji wa Sanaa. Hakukuwa na taarifa kuhusu waliouawa au kujeruhiwa.
Haya yanakuja saa chache kabla ya kuanza kwa utekelezwaji wa mpango wa muda wa kusitisha mapigano kwa masaa 72, unaoanza jumatano hii. Taarifa iliyotolewa na Baraza tawala linalojumuisha waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, na makundi ya kikabila yanayoshirikiana nao, imetaka muungano huo wa majeshi unaoungwa mkono na Saudi Arabia kusimamisha mashambulizi ya kijeshi.
Umoja wa Mataifa umesema mpango huo wa kusitisha mapigano kati ya mahasimu hao unatarajia kuanza saa sita kasoro dakika moja usiku wa jumatano hii kwa saa za Yemen, hatua inayoibua matumaini mapya ya kumalizika kwa vita hivyo vilivyosababisha vifo vya maelfu ya raia na kuacha wengine wakiteseka kwa njaa kali.
Baraza tawala la wahouthi na washirika wao limetangaza kukubaliana na mpango huo wa kusititishwa kwa mapigano kwa kusema Yemen ilihitaji mpango wa haraka na endelevu bila ya kuwepo kwa masharti, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwa vikwazo kwa watu wa Yemen.
Taasisi zinazotoa misaada ya kibinaadamu zitajaribu katika wakati huu wa kusitisha mapigani kuzifikia familia zilizoo kwene maeneo ya miji na vijiji ambapo mapigano kati ya muungano huo na waasi yalisababisha kuwepo kwa vikwazo va kusafiri na kusababisha raia wengi kukosa chakula na mahitaji mengine kama ya dawa.
Mratibu wa masuala ya kibanaadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamie McGoldrick amesema wana imani kwamba mpango huo wa kusitishwa kwa mapigano utawezesha taasisi zinazotoa misaada ya kibinaadamu kuyafikia maeneo ambayo haikuwa rahisi kufikiwa awali.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry amesema, mpango huo uliotangazwa na Mjumbe maalamu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed, unahitaji kuwalazimu makundi hasimu kusitisha shughuli zote ze kijeshi ili kuwezesha kufikishwa kwa misaada.
Mwandishi: Lilian Mtono/Rtre/Dpae.
Mhariri: Daniel Gakuba.