Mapigano yazidi Kongo silaha nzito zikitumika
27 Machi 2026
Licha ya kuondoka kwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kutoka kwenye mji wa Uvira, mapigano bado yanapamba moto kwenye maeneo ya Kivu Kaskazini na Kusini.
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Vivian Van De Perre ametahadharisha kwamba,hali ya usalama huko Kivu Kusini bado ni tete, na mapigano mapya yanaongezeka na kuelekea kwenye mpaka kati ya Kongo na Burundi hali ambayo inaongeza hatari ya kuzuka kwa mgogoro wa kikanda.
Hali jimbo la Ituri inatia hofu
Eneo la Kongo Mashariki limekumbwa na machafuko kwa zaidi ya miongo miwili, huku majeshi ya serikali yakipambana na zaidi ya makundi 100 ya waasi, likiwemo kundi lenye nguvu la M23, ambalo mara nyingi linahusishwa na vita vya kudhibiti madini. Wapiganaji wa M23 walipanua himaya yao mapema mwaka jana, wakiuteka mji wa Goma na miji mingine muhimu.
Van de Perre, anayesimamia kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Congo MONUSCO, chenye takriban wanajeshi 9,000, amesema kuwa hali katika jimbo la Ituri pia inatia hofu,kwani kumekuwa na vifo vingi kutokana na mashambulizi yanayohusishwa na kundi moja la waasi, huku kundi jingine likivamia maeneo ya uchimbaji madini.
Ametaja kuendelea kutanuka kwa mgogoro kutoka eneo la kaskazini hadi kusini mwa Kivu na sasa unaelekea katika jimbo la Tshopo.
Mgogoro wa kibinadamu unazidi kuwa mbaya kutokana na uhaba wa chakula, ambao mwaka 2026 unatarajiwa kuathiri watu milioni 26.6, sawa na takribani robo ya watu wote wa Congo,” alisema Vivian.
Afisa huyo anahofia kwamba,matumizi ya silaha nzito na ndege zisizo na rubani katika miji, linahatarisha maisha ya raia na miundombinu.
Mamlaka ya serikali yamedhoofishwa
Aidha, amesema kuwa M23 imeanzisha mifumo yake ya utawala katika maeneo wanayoyadhibiti, yakiwemo ya Goma, jambo linalodhoofisha mamlaka ya serikali na kufanya utoaji wa misaada kuwa mgumu.Wiki iliyopita, maafisa wa Congo, Rwanda na Marekani walikutana mjini Washington na kukubaliana kuchukua hatua za pamoja kupunguza mvutano mashariki mwa Congo.
Baada ya kikao cha Baraza la Usalama, van de Perre aliwaambia waandishi wa habari kwamba hali "isiyotabirika na yenye hatari kubwa” eneo la mashariki ni sababu ya pande zote kutekeleza makubaliano. Alisema hatua ya kwanza lazima iwe kusitisha mapigano, ikifuatiwa na kufunguliwa tena kwa viwanja vya ndege na kuruhusu walinda amani kusafiri kwa uhuru.
Aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho na mshauri mwandamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika na Kiarabu Massad Boulos, alisema kuwa MONUSCO bado ni muhimu katika kufanikisha mchakato wa amani nchini Kongo.Amesisitiza umuhimu wa pande zote kuheshimu makubaliano yao, ikiwa ni pamoja na kusitishwa kwa vita.