Mapigano yazuka upya Ituri wakati rais Tshisekedi akiwa Goma
14 Juni 2021Akizungumza na waandishi habari katika mji wa Bunia, baada ya waasi wa CODECO kuuteka mji mdogo wa kibiashara wa Fataki, kilomita tisini hivi kaskazini magharibi ya mji wa Bunia mji mkuu wa mkoa wa Ituri, msemaji wa jeshi la serikali katika mko wa Ituri luteni Jules Ngongo alianza kutoa matokeo ya awali ya mapambano hayo kwa matamshi haya.
"Ngao ya jeshi ilikuweko mahala hapo, na tulikabiliana na uvamizi huo na baada ya hapo palikuwa na mapambano ambayo matokeo ni kwamba jeshi liliwapa mkung'uto waasi ambao wamewapoteza wapiganaji wengi, yaani wapiganaji ishirini na mmoja wa CODECO waliouawa, na bunduki tano aina ya AK arubaini na saba tulizichukua toka mikono ya waasi.'' alisema Ngongo.
''Na wanao majeruhi wengi upande wao wanaopatiwa matibabu katika hospitali ya Fataki",aliendelea kusema msemaji huyo wa jeshi.
Hata hivyo duru toka wakaazi wa Fataki zadokeza, kuwa waasi wa CODECO walijiondoa wenyewe kutoka mji huo, na kwamba kuna miili kumi na nne iliyoonekana mjini Fataki,baada ya waasi kuondoka.
Mapambano baina ya jeshi la serikali FARDC na waasi wa CODECO katika wilaya ya Djugu mwishoni mwa wiki iliyopita, yaligharimu maisha ya kanali mmoja wa jeshi, aliyeuawa na CODECO, yeye, mke wake, askari wake walinzi wawili, pamoja na watoto wake wawili kati ya vijiji Katoto na Kparnganza.
Raia wakimbia makazi yao
Mauwaji pamoja na vita kila uchao katika mkoa wa Ituri, hasa katika wilaya ya Irumu, vimeshawapelekea wakaazi wengi kuvihama vijiji vyao na kukimbilia mahala pengine, bila ya msaada wowote.
Hali ngumu ya uchochole wanayoipitia wakimbizi, imempelekea mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika wilaya ya Irumu Guli Gotabo kutoa mwito huu kwa mashirika ya kiutu.
"Tunatoa mwito kwa mashirika ya kiutu kuja kuwahesabu wakimbizi katika maeneo ya Bukiringi, Aveba na idadi ndogo iloyoko hapa Bunia katika jamaa zilizowapokea. Ndio maana tunayaomba mashirika hayo ya kiutu kuja kuwasaidia kwani yasipofanya hivyo, tutashuhudia hali ya utapiamlo hapa. Wilaya ya Irumu ipo katika matatizo, wilaya ya Irumu iko hatarini."
''Nitakwenda Beni kuwapa moyo raia''
Na ili kutathmini hali ya usalama inayojiri katika wilaya ya Beni mkoani Kivu ya Kaskazini, na Bunia mkoani Ituri, rais Félix Antoine Tshisekedi ametangaza kuwa atayazuru maeneo haya hivi karibuni.
Rais aliyasema hayo jana mjini Goma, kwenye mkutano na waandishi wa habari. Huyu hapa rais Félix Antoine Tshisekedi.
"Siku chache zijazo nitakwenda Ituri kutathmini hali inayojiri huko wakati huu wa hali ya dharura. Nitakwenda pia Beni kuwatia moyo raia wa eneo hilo ambao ni wahanga wa vitendo vya ukatili hasa katika viunga vya Beni. Yaani tutakwenda kuwahimiza na kuwaambia kwamba serikali ya Congo haiwezi kamwe kuwasahau na haiwezi kamwe kuachana na vita hadi pale wataapotokomezwa magaidi."
Baada ya Bunia na Beni, rais Félix atauzuru mji mdogo wa Lubiriha, kilomita themanini mashariki ya mji wa Beni, kukutana na rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambako watazindua mradi wa ujenzi wa barabara toka Lubiriha kuja Beni na Butembo.