Mapigano yazuka upya kusini mwa Yemen
26 Agosti 2020Mapigano hayo mapya yalitokea baada ya vuguvugu linaloshinikiza utengano kuacha kushiriki kwenye mazungumzo ya kutekeleza makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Saudi Arabia.
Vuguvugu hilo la Baraza la Mpito la Kusini (STC), ambalo pia ni la wanamgambo wanaoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu, lilisema siku ya Jumanne (Agosti 25) kwamba lilishaiarifu Saudia Arabia hatua yake ya kusitisha mazungumzo, huku likiiaumu serikali ya Rais Abed Mansour Hadi kwa kupeleka vikosi katika mkoa wa kusini wa Abyan.
Hakukuwa na taarifa ya moja kwa moja kutoka kwa serikali ya Hadi. Aidha msemaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika machafuko ya Yemen hakupatikana ili kuzungumzia hali hiyo.
Tangazo la vuguvugu hilo la wanaotaka kujitenga lingeweza kuhujumu juhudi za kumaliza uhasama ambao umedumu kwa mwaka mmoja, mnamo wakati vita vya mpakani dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran vikiendelea.
Vuguvugu la STC lilidai kuwa vikosi vya serikali viliku vimewaua wanamgambo 75 katika mkoa wa Abyan tangu Juni 22, wakati pande zote mbili zilipokubaliana kusitisha vita baada ya miezi kadhaa ya mapigano.
Vuguvugu hilo pia liliishutumu serikali kwa kutolipa mishahara na malipo ya uzeeni katika mikoa ya kusini, hususan kwa maafisa wa kijeshi na walinda usalama wengine.
Mapigano makali mkoani Abyan
Masaa kadhaa baada ya tangazo hilo, mapigano yalizuka usiku kati ya wanamgambo na vikosi vya serikali katika mkoa wa Abyan, ambako muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulipeleka wanajeshi mwezi Juni kuhakikisha makubaliano ya kusitisha vita yanatekelezwa.
Hayo yalithibitishwa na maafisa kutoka pande zote mbili, ambao hawakutaka kutambulishwa kwa kuwa hawaruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari.
Vuguvugu la STC linajumuisha wanamgambo ambao wamejihami kwa silaha nzito nzito na ambao wamekuwa wakishirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu tangu mwaka 2015.
Baraza hilo linatumai kurudisha taifa huru kusini mwa Yemen, ambalo lilikuwepo kutoka mwaka 1967 hadi 1990 wakati ilipoungana na kaskazini kuunga Jamhuri ya Watu ya Yemen chini ya utawala wa Ali Abdallah Saleh.
Makubaliano yavunjika
Kundi hilo lilitangaza utawala wake kwa mji muhimu wa bandari wa Aden pamoja na mikoa mingine ya kusini tangu Aprili, kabla ya kuachana na dhamira yake hiyo mnamo mwezi Julai, ili kutekeleza makubaliano ya amani yaliyokwama kati yao na serikali ya Hadi.
Makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosainiwa katika mji mkuu wa Saudi Arabia, Riyadh, majira yaliyopita ya kiangazi, yalikusudia kumaliza uhasama wa muda mrefu kati ya pande hizo mbili.
Hata hivyo, makubaliano hayo hayakutekelezwa, ikihofiwa kuwa huenda matukio ya hivi yangelihujumu juhudi za kutafuta maelewano katika machafuko ya Yemen.
Yemen ilitumbukia katika machafuko mwaka 2014 wakati waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran walipouvamia mji mkuu Sanaa na maeneo mengine ya kaskazini mwa nchi hiyo na kuilazimisha serikali ya Hadi kukimbilia mafichoni.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia na aunaoungwa mkono na Marekani uliingilia kati machafuko hayo mwaka mmoja baadaye kujaribu kurudisha utawala wa Hadi na kuzuwia ushawishi wa hasimu wake mkubwa, Iran.
Vita hivyo vimeshaangamiza maisha ya zaidi ya watu 112,000 na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekitaja kuwa "janga baya zaidi la kibinadamu ulimwenguni."