1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yazuka upya mjini Tripoli baina ya makundi hasimu

Saleh Mwanamilongo
25 Machi 2020

Mapigano hayo yamezuka upya licha ya mito ya kimataifa kwa ajili usitishwaji mapigano kufuatia kitisho cha mripuko wa ugonjwa wa Corona.

Mpiganaji wa kundi linalounga mkono serikali ya Tripoli,inayotambuliwa na umoja wa mataifa.
Mpiganaji wa kundi linalounga mkono serikali ya Tripoli,inayotambuliwa na umoja wa mataifa.Picha: Imao-Images/Xinhua/A. Salahuddien

Mapigano yamezuka upya mjini Tripoli, Libya baina ya makundi hasimu yanayotaka kuudhibiti mji huo. Kundi la wapiganaji wanaoiunga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa nchini Libya linaelezea kwamba limeshambulia mojawapo ya ngome ya vikosi vya jenerali Khalifa Haftar kusini mwa mji mkuu Tripoli, huku nchi hiyo ikishuhudia kisa cha kwanza cha ugonjwa wa Corona. 

Mapigano hayo yamezuka upya licha ya mito ya kimataifa kwa ajili usitishwaji mapigano kufuatia kitisho cha mripuko wa ugonjwa wa Corona.

Ossama Gowelii, anayeongoza makundi ya wanamgambo yanayoiunga mkono serikali ya mpito amesema kwamba wameshambulia Jumatano ngome ya jeshi la wanaanga la Al-Waitya, inayomilikiwa na wapiganaji wa jenerali Khalifa Haftar, kusini mwa mji wa Tripoli.

Gawelii amesema wapiganaji wake waliivamia ngome hiyo na kuwakamata wapiganaji kadhaa wa Haftar, wakiwemo mamluki kutoka nje, bila kutoa maelezo zaidi.

Kwa upande wao wapiganaji wa jenerali Haftar walikanusha madai hayo na kusema walizuiya mashambulizi hayo waliyoyaita kuwa ni jaribio la kipumbavu.

Mapigano yamekuwa yakiendelea kwa takriban mwaka mmoja sasa baina ya wapiganaji wa jenerali Khalifa Haftar anayeunga mkono serikali ya mashariki mwa Libya na makundi ya wapiganaji yanayounga mkono serikali ya umoja wa kitaifa iliyoko mjini Tripoli na inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

 

 Hofu ya mripuko wa ugonjwa wa Corona

Wiki moja iliyopita makundi hasimu yaliafikia nia ya kusitisha mapigano kwa maslahi ya kiutu, ili kuwaruhusu viongozi kupambana na mripuko wa ugonjwa wa Corona.

Wapiganaji tiifu kwa jenerali Khalifa Haftar wakitembea mjini Bengazi mashariki mwa Libya.Picha: Getty Images/AFP/A. Doma

Kuna hofu kwamba ugonjwa huo unaweza kuiathiri vibaya nchi hiyo iliyo katika vita kwa mwongo mmoja ambao uliharibu miundo mbinu zote muhimu na kusababisha uhaba mkubwa wa dawa.

Tayari kumeripotiwa kisa cha kwanza cha ugonjwa huo nchini Libya, ambako mtu mwenye umri wa miaka 73 aliyeingia Libya kutokea Tunisia, tarehe 5 Machi iliyopita, kulingana na kituo cha kitaifa cha uchunguzi wa maradhi mjini Tripoli.

Ofisi ya umoja wa mataifa ya kuratibu misaada ya kiutu, OCHA, nchini Libya ilielezea leo Jumatano kuwa ina wasiwasi mkubwa, kwamba mripuko wa ugonjwa huo wa Corona utaangamiza vibaya misaada ya kiutu kwa Libya ambayo bado inahitajika zaidi.

 Afya na usalama wa raia wote wa Libya uko hatarini, ilielezea taarifa ya Ocha.

Haftar alianzisha mapigano ya kuuteka mji wa Tripoli mwezi Aprili mwaka uliopita.Hali ya machafuko zaidi imeongezeka miezi ya hivi karibu kufuatia kushiriki kwa vikosi kutoka nje vinavyoyaunga mkono makundi hasimu, licha ya ahadi za mkutano wa kilele uliofanyika mjini Berlin, hapa Ujerumani mapema mwaka huu.

Uturuki imeunga mkono serikali ya Tripoli kwa vifaa vya kijeshi na hata wapiganaji kutoka Syiria, huku Urusi, Misri na Falme za kiarabu zikimuunga mkono jenerali Khalifa Haftar.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW