Mapigano yazuka upya mpaka wa Armenia na Azerbaijan
14 Septemba 2022Wizara ya ulinzi ya Armenia iliituhumu Azerbaijan kwa kurusha makombora, mabomu na kutumia silaha nyengine ndogo ndogo katika mashambulizi hayo mapya, yaliyojiri siku moja tu baada ya kufikiwa makubaliano mapya ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Urusi.
Taarifa ya wizara hiyo ilisema hali kwenye mpaka baina ya nchi hizo mbili bado ni tete.
Kwenye mapigano ya Jumanne (Septemba 13), wanajeshi 49 wa Armenia na 50 wa Azerbaijanwaliuawa wakati mapigano yalipozuka nyakati za alfajiri, huku kila upande ukiulaumu mwengine kwa kuyaanzisha.
Rais Vladimir Putin wa Urusi, ambaye nchi yake ni mshirika wa Armenia, aliingilia kati kwa mazungumzo ya simu kati yake na Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Panishyan, ambaye walikubaliana juu ya usitishaji mapigano.
Azerbaijan iliituhumu Armenia, ambayo ina kituo cha kijeshi cha Urusi, kwa kurusha makombora na mabomu dhidi ya vituo vyake vya kijeshi, ikidai kuwa raia wawili wamejeruhiwa tangu mzozo kuanza.
Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan ilisema kilichofanywa na jeshi lake ilikuwa ni kujibu mashambulizi kwa nia ya kujilinda tu.
Wasiwasi wa kuzuka vita vipya
Mapigano ya sasa yanazuwa wasiwasi wa kutokea vita vyengine vikubwa kwenye eneo la Muungano wa zamani wa Kisovieti wakati huu Urusi inapoendesha vita vyake nchini Ukraine.
Endapo vita kamili kati ya Azerbaijan na Armenia vitazuka, vinaweza kuzishirikisha Urusi na Uturuki, inayoelemea upande wa Azerbaijan, na hivyo kuhatarisha usafirishaji wa mafuta na gesi kama ambavyo vita vya Urusi na Ukraine vimechafua mfumo wa usambazaji chakula na nishati ulimwenguni.
Mbali na Urusi, Marekani, Ufaransa, na Umoja wa Ulaya zimeingilia kati kwa kutowa wito wa kila upande kujizuwia na kuchukuwa hatua zaidi za kijeshi na badala yake kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, aliitaka Urusi kutumia ushawishi wake kutuliza mambo. Hiyo ni baada ya kufanya mazungumzo kwa njia ya simu za Waziri Mkuu wa Armenia, Pashinyan, na Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan.
Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Ulaya, Toivo Klaar, alitazamiwa kuwasilia Caucasus ya Kusini mchana wa Jumatano (Septemba 14) tayari kuanza vikao majadiliano baina ya nchi hizo mbili.
Jumuiya ya Usalama wa Pamoja (CSTO), ambayo Urusi na Armenia ni wanachama, nayo pia ilishatuma ujumbe wake kutathmini hali ilivyo kwenye mpaka wa Nagorno-Karabakh, mkoa ambao kijiografia ni sehemu ya Azerbaijan lakini unakaliwa na watu wa jamii ya Armenia.
Mapigano ya mwaka 2020 kuwania udhibiti wa mkoa huo yalipoteza maisha ya watu zaidi ya 6,500 huku maelfu ya wengine wakigeuka wakimbizi.