1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hali ni tete katika mji wa Mashariki mwa Syria wa Ghouta

9 Machi 2018

Mapigano mapya katika mjini Ghouta,Syria yameiweka hatarini shughuli ya kufikisha misaada katika eneo hilo, wiki tatu baada ya serikali ya Syria kuanzisha mashambulizi mjini humo na kutwaa maeneo yalioshikiliwa na waasi.

Roter Halbmond Syrisch-Arabisch Damaskus
Picha: Getty Images/L. Beshara

Zaidi ya watu 940 wameuwawa tangu Urusi iunge mkono operesheni ya vikosi vya serikali katika ngome zinazoshikiliwa na waasi karibu na mji wa Damascus tarehe 18 Februari. Serikali ya Syria na Urusi zimesema mashambulizi yanayofanyika kwa sasa yanahitajika ili kusitisha yale mashambulizi ya waasi na kumaliza utawala wa kundi la wanamgambo wa dola la kiislamu IS mashariki mwa Ghouta.

Lakini huku hayo yakiarifiwa mashirika ya kutoa misaada ya kiutu imetoa wito wa kuachiwa vifaa vya matibabu kufika katika eneo lililozingirwa la Ghouta, ambapo madaktari na wauguzi wengine wa afya wanapata tabu kuwahudumia mamia ya watu waliojeruhiwa kufuatia kupungua kwa vifaa hivyo.

Watoto mjini Douma wakishuhudia baadhi ya malori ya misaada yakiingia mjini humo Picha: Reuters/B. Khabieh

Kulingana na shirika la uangalizi la haki za binaadamu lililo na makao yake nchini Uingereza, mapema leo asubuhi mashambulizi ya anga yalisimamishwa kwa muda huku eneo hilo kwa mara ya kwanza, likishuhudia ukimya bila mapigano baada ya zaidi ya wiki nzima ya mashambulio ya anga.

Kufuatia ukimya huo, malori 13 ya misaada yaliobeba makontena ya chakula 2,400 yaliingia mjini Ghouta,  hii ikiwa ni kwa mujibu wa Kamati ya Kimataifa ya msalaba mwekundu (ICRC). Muda mfupi baadaye mapigano yakaanza tena katika eneo la Douma baada ya malori hayo kutoka shirika la hilali nyekundu la Syria (SARC)na lile la Umoja wa Mataifa (UN)yalipokuwa yanawasili.

"Makombora yaliyokuwa yanavurumishwa kutoka Douma Mashariki mwa Ghouta yanauweka hatarini msafara wa malori kutoka mashirika ya kadhaa licha ya kuhakikishiwa usalama wao kutoka kwa Urusi,”alisema mratibu wa mipango ya misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Ali al-Zaatari.

Zaatari ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unataka kusimamishwa kwa visa vya kikatili katika eneo hilo na kuomba pia utulivu kuimarishwa nchini Syria. Hata hivyo hakukuwepo na vifaa vya matibabu katika malori yaliyobeba vyakula vilivyoshindwa kufikishwa siku ya Jumatatu.

Baadhi ya vikosi vya Syria Picha: picture-alliance/dpa/C. Huby/Le Pictorium

Zaidi ya watu 340,000 wameuwawa tangu mapigano yalipoanza nchini Syria mwaka 2011 kwa kamata kamata ya waandamanaji wanaoipinga serikali.

Duru nyingi ya mazungumzo yanayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa hayameshindwa kupata suluhu ya mgogoro huo unaoingia mwaka wake wa saba. Mwezi uliyopita wito uliyotolewa na Umoja wa Mataifa wa kusimamisha mapigano haukutekelezwa. Kwa sasa Baraza la Usalama la Umoja huo unatarajiwa kukutana siku ya Jumatatu kusikiliza repoti ya Katibu mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW