Mapinduzi Guinea Bissau
13 Aprili 2012Wanajeshi nchini humo wamevamia makaazi ya Waziri Mkuu usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 13 Aprili na kuwakamata wanasiasa kadhaa. Hadi sasa Waziri Mkuu huyo, Carlos Gomes Junior aliyekuwa anajianda kwa duru ya pili ya uchaguzi hajulikani alipo.
Mapinduzi hayo yametokea ikiwa zimebaki wiki mbili tu kuingia katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais ambao kampeni zake zilikuwa zianze leo na kumalizika tarehe 26 mwezi huu.
Waziri Mkuu Carlos Gomes Junior alishinda duru ya kwanza ya uchaguzi uliofanyika tarehe 18 Machi lakini hakupata kura za kumuwezesha kuepuka duru ya pili ambayo ilitarajiwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu.
Gomes alijaribu kutoroka
Afisa mmoja wa Polisi aliekuwa doria katika makaazi hayo alisema wanajeshi walivamia makaazi ya Gomes kwa gruneti za roketi na kuongeza kuwa wakati hayo yakitokea, Gomes alikuwepo lakini kwa sasa hajui alipo Waziri Mkuu huyo pamoja na Raimundo Pereira, aliyekuwa anakaimu urais wa nchi hiyo baada ya kufariki kwa rais Malam Bacai Sanha, Januari mwaka huu.
Afisa huyo wa polisi alisema Gomes alijaribu kutoka wakati wa purukushani hizo lakini hata yeye hakujua kilichotokea baada ya hapo kwa vile naye alikuwa akijaribu kuokoa maisha yake. Milio ya risasi ilisikika kwa muda wa saa nzima karibu na makaazi hayo ya Waziri mkuu kabla ya kurejea kwa utulivu.
Jeshi lasema linawashikilia wanasiasa
Afisa mmoja wa jeshi ambaye hakutaka kutaja jina lake, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa walikuwa wanamtafuta Carlos Gomes Junior kwa udi na uvumba, na kwamba wangemkamata kabla hakujakucha.
Alisema wanasiasa kadhaa walikamatwa na kupelekwa katika makao makuu ya jeshi mjini Amura, karibu na pwani ya nchi hiyo ingawa haikuweza kufahamika mara moja ni watu gani walikuwa wanashikiliwa na wanajeshi hao.
Wanajeshi walidhibiti makao makuu ya chama tawala na vituo vya redio na televisheni, hali iliyosababisha kukatika kwa matangazo, na pia waliazingira makaazi ya rais lakini hakukuwa na taarifa za maafa yaliyotokana na mapinduzi hayo.
Mji Mkuu, Bissau ulikuwa katika giza kutokana na kukatika kwa umeme na wananchi walilaazimika kukaa ndani ya majumba yao wakati wanajeshi wenye silaha wakirandaranda katika mitaa ya mji huo na kuweka doria nje ya ofisi ya Umoja wa Mataifa na balozi za nje.
Waziri wa mambo ya nje wa Cote D'Ivoire, Daniel Kablan, aliwambia waandishi wa habari baada ya Mkutano wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS kuwa jumuiya hiyo yenye wanachama 15 inlaani mapinduzi hayo na kuwataka wanajeshi hao kuheshimu utawala wa kikatiba.
Guinea na historia ya mapinduzi
Guinea Bissau, ambayo ni koloni la zamani la Ureno ilipata uhuru wake mwaka 1974 baada ya vita vya muda mfupi lakini imekuwa na historia ya mapinduzi.
Mtawala wake wa muda mrefu, Joao Bernardo Vieira alichukua madaraka kwa njia ya mapinduzi mwaka 1980 na kuongoza kwa miaka 19 kabla kupindiliwa mwaka 1999. Alirudi madarakani mwaka 2005 kwa njia ya uchaguzi baada ya kipindi cha kuishi uhamishoni.
Vieira aliuawa na wanajeshi wa Guinea Bissau kwa kupigwa risasi Machi 2009, wakati akikimbia kutoka nyumbani kwake, kufuatia kifo cha mkuu wa majeshi Generali Tagme Na Waie katika mlipuko wa bomu.
Malam Bacai Sanha alishinda uchaguzi wa Julai 2009 lakini alifariki dunia mjini Paris Januari 2012 na Raimundo Pereira alikuwa anakaimu urais hadi mapinduzi hayo yalipotokea.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\AFPE\DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.