Mapinduzi yashindwa Burundi rais ataka maandamano yasitishwe
16 Mei 2015Maandamano yamezuka nchini Burundi katika wiki za hivi karibuni tangu rais Nkurunziza alipoamua kuwania muhula wa tatu madarakani.
Msafara wa magari yaliyomchukua Nkurunziza uliingia katika mji mkuu mapema jana na amerejea katika makao ya rais , amesema msemaji wake, Gervas Abayeho. Rais hakuonekana hadharani.
Wafuasia wake wanaomuunga mkono wakiwa na furaha walishangiria kurejea kwake na kushindwa kwa jaribio hilo la mapinduzi.
Meja jenerali Godefroid Noyombare , mkuu wa zamani wa usalama wa taifa, alitangaza siku ya Jumatano wakati Nkurunziza akiwa nchini Tanzania kwamba amemvua madaraka rais.
Mapigano makali yazuka
Hali hiyo ilizusha mapigano makali katika mji mkuu kati ya majeshi yake na yale tiifu kwa Nkurunziza. Mji huo ulikuwa tulivu lakini hali ni ya wasi wasi jana Ijumaa, ambapo maduka mengi na baishara mbali mbali zilikuwa zimefungwa.
Baadhi ya wakaazi ambao hawaiungi mkono serikali walijitokeza kutoka katika majumba yao na kuanza tena maandamano.
Majenerali watatu wa jeshi wanaoshutumiwa kujaribu kumuangusha kutoka madarakani Nkurunziza wamekamatwa wakati walipopatikana wakiwa wamejificha katika nyumba, wakati afisa mwingine mwandamizi wa usalama alikamatwa mpakani wakati akijaribu kukimbilia nchini Tanzania, Abayeho amesema.
Ameongeza kwamba Niyombare bado hajulikani aliko na msako unaendelea kumkamata.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamewataka maafisa nchini humo kuhakikisha kwamba kampeni ya kulipiza kisasi haifanyiki dhidi ya wale wanaounga mkono mapinduzi na wapinzani wengine wa serikali katika taifa hilo masikini la Afrika ya kati.
Jumuiya ya kimataifa yahimiza kuheshimiwa kwa haki za binadamu
Mjini New York , wanachama wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia wametoa wito wa kurejea kwa haraka kwa utawala wa sheria na mjadala wa kweli kujenga mazingira ya amani, uwazi, ujumuisho na uchaguzi utakaoaminika.
Katika taarifa, pia wameshutumu hususan wale waliosababisha machafuko, na kuwataka maafisa wa Burundi kutatua mzozo huo wakati huo huo wakiheshimu misingi ya uhuru wa kila mtu.
Katika hotuba yake, ambayo iliwekwa katika tovuti yake katika lugha rasmi nchini Burundi ya Kirundi, Nkurunziza amewashukuru majeshi ya ulinzi na ya usalama kwa uwezo waliouonyesha ambapo walipambana dhidi ya waliotaka kufanya mapinduzi dhidi ya taasisi zilizochaguliwa kidemokrasia.
Amesema " amani inatawala nchi nzima, hata mjini Bujumbura ambako kundi dogo la wahalifu lilitaka kutenda kitu ambacho hakingeweza kurekebishwa," akimaanisha waliopanga mapinduzi , na akaongeza kuwa walikuwa wanatayarisha hatua hiyo , "kwa muda mrefu , tangu mwaka jana na kabla ya hapo."
Nkurunziza ametoa wito wa kumalizika mara moja kwa uhasama na ametaka kufanyike mjadala.
"Tunahimiza kwa hiyo kusitishwa mara moja kwa maandamano, na wale wenye madai watafanya hivyo katika mjadala, na sio kwa kutumia nguvu na uasi," ameongeza.
Maandamano yalianza Aprili 26 , siku moja baada ya chama tawala kumtangaza Nkurunziza kuwa mgombea wake katika uchaguzi, na watu 15 wameuwawa katika ghasia hizo.
Katiba inasema kwamba rais anaweza kuchaguliwa na umma kwa vipindi viwili, lakini Nkurunziza anadai kuwa anaweza kugombea tena kwasababu alichaguliwa na bunge kuwa rais katika kipindi cha kwanza, akiwa na nafasi ya kuchaguliwa na umma kwa vipindi viwili.
Wapinzani wanasema mpango wake unakiuka katiba pamoja na makubaliano ya amani ambayo yalifikisha mwisho vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Zaidi ya Warundi 105,000 wameikimbia nchi hiyo na kwenda katika nchi jirani hivi karibuni , kwa mujibu wa Umoja wa mataifa , na kamishina wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR Zeid Ra'ad Al Hussein ameonya jana kuwa nchi hiyo imo katika hatari ya kutumbukia zaidi katika ghasia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Idd Ssessanga