1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maporomoko ya theluji yaua mamia Kashmir

14 Januari 2020

Maporomoko ya ardhi, mafuriko na hali mbaya ya hewa kwa pamoja vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 130 kote nchini Pakistan na Afghanistan katika siku za hivi karibun.

Kaschmir Lawine in Neelum Valley
Picha: Getty Images/AFP

Kulingana na maafisa wa mataifa hayo mawili, takriban watu 93 wamekufa na wengine 76 wamejeruhiwa nchini Pakistan lakini pia baadhi wakiwa hawajulikani walipo. Watu 39 wamekufa nchini Afghanistan.

06.01.2020 Matangazo ya Jioni

This browser does not support the audio element.

Utabiri wa hali ya hewa unaonyesha hali mbaya zaidi itayakabili maeneo hayo hivi karibuni.

Jimbo la Kashmir nchini Pakistan ndilo lililoathirika zaidi na hali hiyo ikilinganishwa na maeneo mengine. Taarifa ya mamlaka ya kupambana na majanga imesema watu 62 wamekufa na wengine 10 wamepotea.

Maporomoko ya mara kwa mara ya theluji na udongo hutokea kwenye jimbo la Kashmir nyakati za baridi, na mara nyingi huzuia barabara na kuzitenganisha jamii za eneo hilo. Mamlaka zimezifunga shule wakati baadhi ya barabara kuu zikiwa zimefungwa katika eneo lote la milimani lililoko kaskazini mwa Pakistan.

Hali ya hewa Afghanistan ni mbaya na kusababisha majanga makubwaPicha: DW/S. Tanha

Waziri mkuu wa Pakistan Imrah Khan ameandika kwenye ukurasa wa twitter akisema maporomoko kwenye eneo la Kashmir linalotawaliwa na Pakistan, yamesababisha hofu kuu na vifo.

Kwenye jimbo la Balochistan lililopo kusinimashariki, takriban watu 31 wamekufa katika matukio tofauti tofauti yanayohusiana na hali hiyo mbaya ya hewa. Afisa anayehusika na majanga kwenye eneo hilo Mohammad Younus amesema wengi miongoni mwao walikuwa ni wanawake na watoto, na wengi wakiwa bado wamekwama.

Msemaji wa mamlaka ya majanga ya asili Tamim Azimi amesema zaidi ya nyumba 300  zimeharibiwa kabisa ama kwa kiasi katika ameneo mengi nchini humo. Amesema baridi kali, mvua kubwa na theluji vimeanza wiki mbili zilizopita na kwa pamoja vimesababisha majanga makubwa. Amesema majanga zaidi yalisababishwa na theluji kubwa kuangukia nyumba.

Jimbo la kashmir limetangaza hali ya dharura kwenye maeneo yaliyoathirika mapema hii leo, hii ikiwa ni kulingana na waziri wa mamlaka inayoshughulikia majanga Ahmad Raza Qadri.

Vikosi vya uokozi navyo vinakabiliwa na changamoto kubwa ya namna ya kuwafikia watu waliokwama na waokozi pia wamelazimika kutumia helikopta.

Baadhi ya maeneo ya Pakistan yamefunikwa na theluji kwa inchi sita na hali ya hewa hapo jana ikifikia nyuzi joto -15 Celcius.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW