MAPUTO : Chissano ajiuzulu uenyekiti wa FRELIMO
6 Machi 2005Kiongozi wa zamani wa Msumbiji Joaquim Chissano amejiuzulu wadhifa wake wa mwenyekiti wa chama tawala nchini humo na kuthibitisha kile wazaidizi wake wanachosema kutotaka kuwa na dhima yoyote ile katika siasa za nchi hiyo aliyoitawala kwa miaka 18.
Mfanya biashara Armando Guebuza ambaye alichukuwa nafasi ya Chissano kama Rais wa taifa hilo mwezi uliopita baada ya kushinda uchaguzi wa Urais wa mwezi wa Desemba mwaka 2004 ametangazwa kuwa Mwenyekiti mpya wa chama cha Ukombozi wa Msumbiji FRELIMO.
Kwa mujibu wa msaidizi wake mwandamizi Chissano ameamuwa kujiuzulu ili kumpa nafasi Guebuza kupitisha sera zake kupitia vitengo vya FRELIMO na kwamba Chissano mwenye umri wa miaka 68 alikuwa hataki kuonekana kama anamkwamisha Guebuza kuifanyia mageuzi nchi hiyo.
Guebuza mwenye umri wa miaka 61 ameahidi kuendeleza mafanikio ya uchumi yaliyopatikana chini ya uongozi wa Chissano na pia kupiga vita rushwa,uhalifu na kushughulikia miundo mbinu ili kupunguza umaskini.