Marco Rubio akutana na mawaziri wenzake wa G7 kujadili Iran
27 Machi 2026
Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika, tangu Marekani ambae ni mwanachama wa G7 kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran. Vita vya Iran vinatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika ajenda ya mkutano huo.
Rubio anatarajiwa kujibu maswali mazito kutoka kwa washirika wake wa Ulaya kuhusu mkakati wa Marekani katika Vita hivyo vilivyoanza Februari 28 ambayo tayari vimesababisha bei ya mafuta kupanda duniani kutokana na mlango bahari wa Hormuz kufungwa na Iran. Mlango huo unatumika kusafirishia asilimia 20 ya nishati ya mafuta duniani.
Uingereza: Uhusiano wa Urusi na Iran unatupa mashaka
Huku hayo yakiarifiwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza Yvette Cooper nchi yake na washirika wake wa G7 wanawasiwasi kuhusu mafungamano ya Urusi na Iran baada ya ya nchi za Magharibi kuituhumu Moscow kuisaidia Tehran kushambulia vituo vya Marekani katikaeneo la Ghuba.
"Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu uhusiano kati ya Urusi na Iran ambao ni wa muda mrefu - kama vile Iran inavyoipa Urusi droni zinazotumika kwenye vita vya Ukraine. Lakini pia tumeona jinsi Urusi inavyoisaidia Iran katika mzozo wa Mashariki ya Kati. Na ndiyo maana G7, tumekuja pamoja kujadili mambo haya na njia ya kuulinda uchumi wa dunia kutoka nchi zinazotaka kutumia silaha kuathiri uchumi wetu"
Urusi imekanusha vikali tuhuma hizo. Mkutano unaofanyika nje ya Paris utavijadili pia vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, hali ya Mashariki ya Kati, pamoja na vitisho vinavyoikabili amani na utulivu wa duniani.