1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Baraza la seneti lamwondolea mashtaka Donald Trump

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
14 Februari 2021

Baraza la seneti nchini Marekani limemwondolea mashtaka rais wa hapo awali Donald Trump. Mashtaka hayo yalihusu kuchochea maasi na uvamizi wa bunge baada ya Trump kushindwa katika uchaguzi.

USA Impeachment Trump Senat
Picha: Senate Television/AP Photo/picture alliance

Maseneta 57 walipiga kura ya kumtia hatiani rais huyo wa zamani na 43 waliyakaa mashtaka dhidi yake.Wajumbe saba  wa chama cha Republican waliungana na wajumbe wa chama cha Democratic kumtia hatiani Trump, lakini idadi hiyo haikufikia  theluthi mbili iliyohitajika.

Kiongozi wa maseneta wa chama cha Republican Mitch McConell amesema ni wazi kabisa kwamba Donald Trump alihusika na kuchochea mashambulio kwenye bunge. Hata hivyo hakupiga kura ya kumtia hatiani rais huyo wa hapo awali.

Rais wa zamani wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/J. Ernst

McConell ameeleza kuwa kwa mujibu wa katiba hastahiki kushtakiwa kwa sababu sasa hayumo tena madarakani, hata hivyo Mitch McConnell amesema hakuna tashwishi kwamba Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amekosea katika majukumu ya kiuadilifu na kimaadili kwa kuchochea vurugu mbaya mwezi uliopita.

Matokeo ya Trump kuondolewa mashtaka kumesababisha migawanyiko ya utata nchini Marekani kuhusiana na siasa za Trump zilizosababisha maasi dhidi ya mmoja ya mihimili mitatu ya demokrasia ya Marekani.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo kutolewa rais Joe Biden amesema kipindi hiki cha kusikitisha katika historia ya Marekani kinatukumbusha kwamba demokrasia ni jambo nyeti. Biden amesea ingawa Trump hakutiwa hatiani, kiini cha mashtaka hakiwezi kukanushwa.

Chanzo:AP