1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani:Baraza la Seneti lapitisha mpango wa kufufua uchumi

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
7 Machi 2021

Baraza la Seneti la nchini Marekani limepiga kura kuidhinisha mpango mkubwa wa msaada wa fedha wa trilioni 1.9 ambazo Rais Joe Biden amesema zitasaidia kuufufua uchumi.

USA | Washington | Abstimmung im Senat
Picha: Senate Television/AP Photo/picture alliance

Wajumbe wa chama cha Democratic katika Baraza la Seneti walifanikiwa kupiga kura na kuupitisha muswada wa mpango huo wa misaada ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia wafanyakazi na wafanyabiashara walioathiriwa vibaya na janga la virusi vya corona.

Muswada huo uliidhinishwa kwa kuzingatia misingi ya vyama baada ya zoezi refu zaidi la upigaji kura katika historia ya siasa za nchini Marekani. Ilichukua muda wa saa 12 mpaka yalipopatikana maelewano miongoni mwa wanachama wa chama cha Democratic kwa ajili ya kumshawishi Seneta mwenye msimamo wa kihafidhina Joe Manchin, ambaye alikuwa anapinga kiwango cha fidia kinachopangwa kutolewa kwa watu wasio na ajira.

Muswada huo wa jumla ya dola trilioni 1.9 za misaada ya kifedha sasa utarudishwa kwenye Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kupitishwa na kuwa sheria. Baada ya hapo utaweza kusainiwa na Rais Joe Biden.

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Rais Biden anataka mpango huo mkubwa wa fedha usaidie kuufufua uchumi wa nchi yake na kuwezesha kupatikana mamilioni ya nafasi za ajira mpya. Miongoni mwa mambo mengine, muswada huo utawawezesha Wamarekani wengi wanaolipa kodi kupatiwa moja kwa moja kiasi cha dola 1,400.

Muswada huo, maarufu miongoni mwa wapiga kura wa Marekani, umekuwa ni wa kipaumbele kwa utawala wa rais Joe Biden.

Watu milioni 9.5 walipoteza kazi mwaka uliopita wa 2020 wakati janga la maambukizi ya virusi vya corona lilipotokea. Ikulu ya Marekani imesema itachukua miaka kadhaa hadi kuisawazisha hali hiyo ya ukosefu wa ajira. Hata hivyo, takwimu za nwishoni mwa wiki zilionyesha kuwa nafasi mpya za ajira zipatazo 379,000 ziliongezeka mnamo mwezi Februari, kiwango hicho kizuri hakikutarajiwa na wachumi.

Kiongozi wa Baraza la Seneti wa chama cha Democrats Chuck SchumerPicha: picture-alliance/CNP/S. Reynolds

Baraza la Seneti liliupitisha muswada huo kura 50 za ndio huku kura 49 zikiwa zinaupinga. Wademocrat walipata ushindi huo finyu baada ya Seneta wa chama cha Republican wa jimbo la Alaska, Daniel Sullivan kutoshiriki kwenye kura hiyo kutokana na kulazimika kwenda kuhudhuria mazishi ya mwanafamilia, ikimaanisha kwamba Makamu wa Rais Kamala Harris hakulazimika kuingilia kati na kupiga kura yake ili kukipa ushindi chama chake. Baraza la Seneti lina wajumbe 50 wa chama cha Democtratic na chama cha Republican pia kina jumla ya wajumbe 50.

Rais Joe Biden amempongeza kiongozi wa Baraza la Seneti, Chuck Schumer na wajumbe wengine wa baraza hilo wa chama cha Democratic kwa hatua hiyo kubwa iliyofikiwa ambayo inafungua njia ya kuendelea mbele na ajenda za chama cha Democratic, lakini kiongozi wa chama cha Republican Mitch McConnell, kilicho na wajumbe wachache kwenye Baraza la Seneti hakuisherehekea hatua hiyo, amesema Baraza la Seneti halijawahi kutumia fedha nyingi namna hiyo na kwa mtazamo wake fedha hizo zitatumika kwa njia mbaya.

Vyanzo:/AFP/AP/https://p.dw.com/p/3qJID