Marekani- China zatunishiana misuli teknolojia ya AI
2 Februari 2026
Mwaka mmoja uliopita katika wiki kama hii,eneo la Marekani la matumizi na uvumbuzi wa teknolojia ya hali ya juu Silicon Valley na eneo la biashara muhimu la Wall Street yalishtushwa na uzinduzi wa app mpya ya China ya DeepSeek ambayo inapambana na zile za Marekani za mawasiliano mfanoChat GPT, kwa kubainisha utendaji wa hali ya juu kwa gharama ndogo zaidi na matumizi ya teknolojia ya chini zaidi.
DeepSeek imefungua ukurasa mpya wa uhasama wa kibiashara kati ya China na Marekani, huku ulimwengu ukitambua ushindani wa bidhaa hizo na Beijing yenyewe ikiwekeza zaidi kwenye juhudi za kuunda mfumo binafsi wa akili mnemba.
Miezi kadhaa baada ya DeepSeek kuzinduliwa,uongozi wa rais Donald Trump wa Marekani ulibainisha kuwa uko mbioni kuwa mstari wa mbele na kuitawala sekta ya akili mnemba AI, duniani.
Mpango huo ujilikanao kama "kuzishinda mbio za AI,” unatoa wito wa kufutilia mbali vikwazo vinavyodaiwa kuwekea vizingiti uzinduzi na kuiweka teknolojia ya Marekani kwenye nafasi ya mbele katika jukwaa na kilimwengu.
Kimsingi, mataifa yote yanayonuwia kujiunga na muungano wa Marekani wa jeshi la Akili mnemba sharti washirikiane nao kwa hali zote za teknolojia ikiwemo mifumo,programu,maunzi na vigezo ili kuwazuwia washindani wake wa biashara kutegemea teknolojia ya kigeni kutekeleza uhasama au kutishia uwepo wake kwenye sekta hiyo.
Mpango wa Akili Mnemba wa China
Wakati huo huo, Beijing nayo ilichapisha mpango wake wa kimataifa wa akili mnemba unaoshajiisha uwazi, uvumbuzi na ushirikiano wa mfumo wa akili mnemba utakaowaleta pamoja wadau mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ubadilishanaji wa mawazo na majadiliano ya usimamizi wa teknolojia hiyo.
Scott Singer aliyezungumza na DW ni mtaalam katika mpango wa teknolojia na masuala ya kimataifa kwenye taasisi ya utafiti ya Carnegie Endowment for International Peace, na anamini kuwa China inajiweka katika nafasi ambapo iko wazi na tayari kwa ushirikiano kama mdau wa kimataifa anayejikita katika maendeleo.
Ijapokuwa appu kama DeepSeek na nyengine za mawasiliiano za China zina umaarufu,na utendaji wake uko kwenye daraja moja na OpenAl au Gemini kutumua ujumbe, kutafsiri na uelekezi,bado wataalam wa teknolojia wa Marekani wataendelea kuwa mstari wa mbele. Chipu zinazotumia teknolojia ya hali ya juu zinatengezwa na Nvidia iliyoko Silicon Valley, na Marekani iko mbele sana ya China kwenye ufundi huo.
China ina utajiri wa ujuzi wa akili mnemba, data kwa wingi na rasilmali za nishati ila inakosa kiungo muhimu nacho ni chipu za teknolojia ya hali ya juu zinazohitajika kwenye mifumo ya kompyuta.
Marekani ina udhibiti mkali wa uuzaji nje wa chipu hizo. Huawei Ascend ndiyo inayotengeza chipu za hali ya juu za akili mnemba.
Hata hivyo, Huawei haina uwezo wa kutengeza idadi kubwa ya chipu kama Nvidia ya Marekani kwahiyo ushirikiano wa kiteknolojia kuimarisha utendaji utazua changamoto za gharama na ufundi.
Mabadiliko ya kisera kuhusu teknolojia Marekani
Mwezi Disemba mwaka uliopita,uongozi wa Trump ulibainisha kuwa umebadili sera kwa kuridhia uuzaji wa chipu maalum za Nvidia kwa wanunuzi walioteuliwa wa China kwa manufaa ya kupata sehemu ya mapato yake.
Kimsingi Marekani inaisukuma China kukumbatia teknolojia yake ya zamani ya akili mnemba ili isalie kwenye mstari wa mbele.
Wakosoaji wanatahadharisha kuwa teknolojia hiyo bado ina uwezo mkubwa na huenda ikapiga hatua na kuipiku Marekani. Kwa sasa chipu hizo zinazuiliwa kuingia China. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kampuni za China zimeagizwa kutonunua chipu hizo ila haijakuwa bayana hilo litaendelea kwa muda gani.
Kampuni za China za Alibaba,Tencent,ByteDance zilikuwa tayari zimeagizia chipu zaidi ya milioni 2 kwa thamani ya euro bilioni 43.
Hata hivyo,mfumo wa akili mnemba wa China unanawiri na appu zake zinazinduliwa kwa gharama ya chini zaidi na vikwazo vichache zaidi.
Kweney ujumbe wake wa mwaka mpya,rais wa China Xi Jinping alibainisha kuwa mwaka 2025,teknolojia yao ilikwea na kufikia viwango vya juu.
Ufanisi wa China kwenye sekta hiyo umeisukuma azma ya Beijing ya kuzindua mfumo wa akili mnemba unaozipa kipaumbele suluhu za hapo kwa papo za changamoto za maisha mfano matumizi ya robot na kwenye sekta ya viwanda.
Kwa ufupi Marekani inajikita zaidi katika kuimarisha programu na kuwezesha matumizi ya kompyuta kwa wigo mpana zaidi.
China kwa upande wake,inawekeza katika mifumo ya robotiki inayoendeshwa na nguvu ya akili mnemba.