Marekani, Cuba zapiga hatua mpya kwenye uhusiano
10 Aprili 2015Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mazungumzo kati ya John Kerry na mwenzake wa Cuba, Bruno Rodriguez, ambayo ni ya kwanza kabisa tangu mwaka 1958, yalikwenda vyema.
"Mawaziri Kerry na Rodriguez walikuwa na majadiliano marefu na ya msingi sana. Wamekubali kuwa wamepiga hatua kubwa na tutaendelea kushirikiana kuyatatua masuala yaliyobakia," ilisema taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nje ya Marekani, ambayo kwenye mtandao wake wa Twitter ilichapisha picha inayowaonesha Kerry na Rodriguez wakipeana mikono.
Rais Barack Obama na mwenzake Raul Castro waliwasili masaa kadhaa kabla ya kuanza kwa mkutano wa kilele wa mataifa ya Amerika hivi leo, ambapo nao pia wamepangiwa kukutana uso kwa uso, ikiwa ni sehemu ya kurejesha upya mahusiano kati ya nchi zao yaliyovunjika tangu mwaka 1961.
Obama anatajwa kusogelea zaidi kwenye hatua za kuondoa kikwazo kikubwa cha kidiplomasia, baada ya Seneta Ben Cardin wa Kamati ya Mambo ya Nje kusema kuwa Kerry alipendekeza serikali ya Cuba iondolewe kwenye orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi. Seneta Cardin amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuendeleza juhudi zitakazozaa uhusiano wenye faida na Cuba.
Kikwazo cha kuwamo kwenye orodha
Wakati wa ziara yake nchini Jamaica akiwa njiani kuelekea Panama, Obama alithibitisha kwamba tayari Wizara ya Mambo ya Nje ilishakamilisha uhakiki wa Cuba kwenye orodha hiyo, ingawa alikataa kusema kilichopendekezwa.
Kuendelea kuwa na jina la Cuba kwenye orodha hiyo kumekuwa kigingi kikubwa katika majadiliano yanayoendelea, ambayo yanadhamiriwa kuwezesha kufunguliwa kwa balozi za nchi hizo zilizofungwa zaidi ya nusu karne sasa.
Kuwekwa kwenye orodha hiyo kulimaanisha kwamba Cuba ilistahili kuwekewa vikwazo vya silaha na misaada ya kiuchumi na pia vikwazo vya kifedha, ambavyo vinaifanya ishindwe kupata mikopo kutoka Benki ya Dunia na taasisi nyengine za kifedha.
Kwa mara ya kwanza Cuba iliwekwa kwenye orodha hiyo mwaka 1982 kwa kuwahifadhi waasi wa ETA wanaotaka kujitenga kwa jimbo la Basque kutoka Uhispania, na wale wa FARC nchini Colombia. Kwenye orodha hiyo, zimo pia Syria, Sudan na Iran.
Hii pia ni mara ya kwanza kwa Cuba kuhudhuria mkutano huu wa kilele wa mabara ya Amerika, jukwaa linalozikutanisha nchi za Amerika ya Kaskazini na ya Kusini.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba