Marekani haina budi kufanya kazi na Kenyatta
12 Machi 2013 Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani, John Kerry aliwapongeza watu wa Kenya kwa kufanya uchaguzi wa amani lakini kamwe hakulitaja hata mara moja jina la Kenyatta katika pongezi hizo. zake.
Licha ya hayo, hata hivyo, serikali ya Kenya haina haja ya kuwa na wasiwasi, kwa sababu mashirika ya usalama ya nchi mbili hizo yanashirikiana katika harakati za kupambana na ugaidi na, kwa ajili hiyo, Kenya inapatiwa msaada upatao dola bilioni 1 kila mwaka.
Hata hivyo, mara tu baada ya mshindi wa uchaguzi nchini Kenya kutangazwa, redio ya taifa ya Marekani ilitilia maanani kuwa Kenyatta anakabiliwa siyo tu na kesi ya udanganyifu wa kura, bali pia rais huyo mteule na makamu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashtaka mbele ya ICC.
Marekani haina njia ila kushirikiana na Kenyatta
Ushindi wa Kenyatta sio tu umezua hali mpya katika sheria za kimataifa, bali utata katika jumuiya ya kimataifa linapohusika suala la mahusiano ya kidiplomasia.
Hata hivyo, kwa mujibu wa tathmini ya vyombo vya habari mashuhuri nchini Marekani, ikiwa pamoja na magazeti ya New York Times na Washington Post redio maarufu ya NPR, utawala wa Rais Barack Obama hauna njia nyingine ila kushirikiana kwa undani na washtakiwa hao wawili watakaokuwa viongozi wakuu katika serikali ya Kenya.
Mjumbe wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Johnny Carson, aliyewahi kuwa balozi wa Marekani nchini Kenya, aliwatahadharisha wazi Wakenya dhidi ya kumpa kura Kenyatta anayekabiliwa na mashtaka mbele ya ICC, na serikali ya Marekani ilijaribu mapema kufanya kila iwezalp kuzuia uwezekano wowote wa udanganyifu wa kura.
Utawala wa Obama ulitenga haraka kiasi cha dola milioni 37 kwa ajili ya mafunzo ya maafisa wa kusimamia uchaguzi nchini Kenya na pia kwa ajili ya kugharimia kompyuta za uchaguzi.
Ilishindwa kumzuia, sasa yapaswa kumvumilia
Lakini sasa baada ya juhudi zote za Marekani za kumzuia Kenyatta anayekabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kuwa rais kushindikana, utawala wa Obama unalazimika kushirikiana na rais huyo mteule.
Kwa mtazamo wa Marekani, Kenya ni muhimu siyo tu kutokana na kuwa nchi ya tatu duniani kwa makao ya Umoja wa Mataifa, baada ya New York na Geneva, bali pia ni mshirika muhimu sana wa Marekani katika harakati za kupambana na ugaidi barani Afrika.
Ndiyo sababu kwamba Marekani imejenga ubalozi wake mkubwa kuliko kwingineko kote kusini mwa jangwa la Sahara nchini Kenya. Ubalozi huo pia ni kituo muhimu cha Shirika la Ujasusi (CIA), kwani Marekani haitayasahau mashambulizi yaliyofanywa na magaidi kwenye balozi zake za Kenya na Tanzania.
Pia mmoja wa washambuliaji wa ubalozi wa Marekani nchini Kenya alikuwa miongoni mwa magaidi walioyaandaa mashambulizi ya tarehe 11 Septemba 2001.
Kenya pia ni kituo muhimu kwa operesheni za Marekani katika kuwadhibiti Waislamu wenye itikadi kali nchini Somalia. Kwa hiyo kwa tathmini ya vyombovya habari vya Marekani "itakuwa vigumu kiwekea nchi kama Kenya vikwazo."
Vyombo vya habari vya Marekani vinasema pia itakuwa vigumu kwa utawala wa Obama kukataa kushirikiana na Kenyatta ati kwa sababu ya kukabiliwa na mashtaka kwenye Mahakama Kuu ya The Hague, ambayo yenyewe Marekani haiitambui.
Mwandishi: Ralph Sina
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Khelef