1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani iko tayari kuiunga mkono Georgia

Kabogo Grace Patricia24 Julai 2009

Msisitizo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden katika ziara yake mjini Tbilisi.

Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden.Picha: AP


Baada ya vita kati ya Urusi na Georgia, Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden, ameihakikishia Georgia kuwa Marekani iko tayari kuiunga mkono Georgia, jimbo la zamani la Urusi. Kauli hiyo ameitoa katika ziara yake katika mji mkuu wa Georgia, Tbilisi.

Joe Biden amesisitiza kuwa Marekani iko tayari kumaliza mzozo uliopo baina ya Urusi na Georgia, huku akiitaka Urusi kuyaondoa majeshi yake yaliyoko kwenye majimbo mawili ya Georgia, ambayo ni Abkhazia na Ossetia ya Kusini. Hata hivyo, Joe Biden ameitaka Georgia kutodai kurejeshwa kwa majimbo yake hayo kwa kutumia nguvu.

Aidha, makamu huyo wa rais wa Marekani ameitaka Georgia kuimarisha demokrasia, miaka sita baada ya mapinduzi ya amani ya waridi yaliyoondoa utawala wa Kisovieti na kumuweka madarakani Rais Mikhail Saakashvili.

Katika hotuba yake kwa Bunge la Georgia, Joe Biden amesema nchi yake inaunga mkono juhudi za Georgia kujiunga na Umoja wa NATO, hatua inayopingwa vikali na Urusi na kusema kuwa Georgia ni moja kati ya nchi zinazopokea msaada mkubwa kutoka Marekani. Wakati Biden amekutana na Saakashvili, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi, Grigory Karasin, ameonya kuwa Urusi haitairuhusu Georgia kuwa tena na silaha, kufuatia vita vya siku tano vya mwezi Agosti, mwaka uliopita, ambapo majeshi yake mengi yaliharibiwa. Joe Biden amekiri kuwa Marekani inaisadia Georgia katika masuala ya kijeshi, lakini amesema jitihada hizo ni pamoja na mipangilio na mafunzo ya kijeshi, lakini siyo kusambaza silaha.

Maafisa wa Georgia wamesema kuwa mpango wa Marekani wa kusambaza silaha kwa Georgia, haukuzungumziwa katika mikutano ya Joe Biden. Georgia inatafuta msaada wa Marekani katika kutatua mzozo wa eneo hilo, ambapo imependekeza itume waangalizi kujiunga na wale wa Umoja wa Ulaya kuangalia makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yanalegalega katika mpaka wa Georgia na majimbo mawili ya nchi hiyo yaliyojitenga ya Ossetia Kusini na Abkhazia.

Kwa upande wao, wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema bado haijajulikana ni kiasi gani Rais Barack Obama wa Marekani amejiandaa kuisadia Georgia, bila kuelezea aina ya ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.

Mwezi Januari mwaka huu, Marekani na Georgia zilisaini mkataba wa ushirikiano uliohusisha mipango ya kutoa mafunzo na kuyapa silaha majeshi ya Georgia, lengo likiwa nchi hiyo kuongeza uwezo wake wa kufanya kazi na majeshi ya NATO. Makubaliano hayo yalisainiwa na Waziri wa zamani wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, na mwenzake wa Georgia, Grigol Vashadze.

Ziara ya Bwana Biden nchini Georgia inafanyika ikiwa karibu mwaka mmoja tangu nchi hiyo ilipoingia katika vita vya siku tano na Urusi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE)

Mhariri: Miraji Othman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW