1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani iko tayari kuzungumza na Iran

Amina Abubakar Yusuf Saumu
25 Juni 2019

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani John Bolton amesema rais wa nchi hiyo Donald Trump amefungua mlango wa majadiliano ya kweli kati ya nchi hiyo na Iran. Marekani imetoa tamko hilo huku ikiiwekea vikwazo vipya Iran.

USA Washington Donald Trump unterschreibt Executive Order zu Iran
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

 

John Bolton amesema kile Iran inachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuingia kupitia mlango wa majadiliano uliyowachwa wazi na Marekani ili kutafuta suluhu ya mvutano unaoendelea.

Hata hivyo balozi wa Marekani anayesimamia masuala ya kupunguza silaha Robert Woods amesema nchi hiyo itaendelea na shinikizo lake dhidi ya  Iran hadi itakapobadilisha tabia yake. Marekani imeongeza kuwa itatafuta njia tofauti za kuiongezea vikwazo zaidi Iran.

Mshauri wa Usalama wa taifa wa Marekani John Bolton Picha: Getty Images/A. Wong

Iran kwa upande wake imepuuzia vikwazo hivyo vipya ilivyowekewa na Marekani. Wanachama wa bunge la nchi hiyo wamesema mbinu ya Marekeni haifai, kutaka mazungumzo mapya  huku ikiiiwekea vikwazo Iran, kiongozi wake wa kidini Ayatolla Ali Khamenei pamoja na maafisa wengine wanne wa juu serikalini na vikwazo zaidi dhidi ya waziri wa mambo ya kigeni Javad Zarif vikitarajiwa kuwekwa baadae wiki hii.

Rais Hassan Rouhani amesema vikwazo dhidi ya Khamenei havitakuwa na athari yoyote

Mvutano kati ya Iran na Marekani umepamba moto baada ya Irankuidungua wiki iliyopita ndege isiyokuwa na Rubani ya Marekani na Trump kuzuwiya mashambulizi ya kijeshi katika dakika ya mwisho akihofia watu zaidi watauwawa.

Pindi shambulio hilo lingefanyika basi ingekuwa mara ya kwanza Marekani kuishambulia kijeshi Iran katika kipindi cha muda mrefu wa uadui kati yao.

Rais wa Iran Hassan Rouhani Picha: picture-alliance/abaca/Parspix

Kwa upande wake Rais Hassan Rouhani amesema vikwazo dhidi ya Khamenei havitakuwa na athari yoyote maana kiongozi huyo wa kidini hana mali yoyote katika nchi za Magharibi.

Iran na Marekani wamezidi kukwaruzana tangu mwaka uliopita wakati rais Trump alipoiondoa nchi yake katika  makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa sita yaliyo na nguvu duniani kabla ya Marekani kuiwekea tena vikwazo nchi hiyo.

Wakati huo huo Urusi imeishutumu Marekani kuwa mwepesi kuiwekea Iran vikwazo bila kufikiria huku ikitangaza kusimama pamoja na Iran. Urusi imesema kuna hisia zinazoonesha, Marekani inataka kusitisha kabisa uhusiano wake na Iran.

Vyanzo: Reuters/AFP/AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW