Marekani imewatambua waasi Libya
16 Julai 2011Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton alitangaza hayo katika mkutano mjini Istanbul Uturuki, wa zaidi ya mataifa 30 na taasisi za kimataifa, zijulikanazo kama kundi la mashauriano kuhusu Libya. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague amesema kundi hilo liliahidi kuwaunga mkono waasi hao katika jitihada zao za kutaka kumuondoa uongozini Muammer Gaddafi.
Kutambuliwa baraza hilo la waasi huenda kukasababisha kutolewa fedha nyingi. Uturuki imesema dola bilioni 3 za mali ya Libya zilizozuiliwa zitatolewa , ili muradi fedha hizo zitumike kwa sababu za kibinadamu pekee. Makubaliano ya baraza la usalama la Umoja wa mataifa pamoja na vikwazo vya kimataifa dhidi ya utawala wa Gaddafi, vimezuia fedha za Libya katika nchi za nje. Gaddafi anakataa kujiuzulu na amesema atapigana hadi mwisho.
Mwandishi: Maryam Abdalla,AFP, dpa, Reuters
Mhariri: Kitojo,Sekione