1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Netanyahu apanga 'tarehe' ya kuivamia Rafah

9 Aprili 2024

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema tayari wameshapanga tarehe ya kuuuvamia mji wa Rafah, siku moja baada ya jeshi la nchi hiyo kusema limepunguza wanajeshi wake waliokuwa kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametangaza kwamba tayari amepanga tarehe ya kuivamia kijeshi RafahPicha: Ronen Zvulun/AP Photo/picture alliance

Marekani imekosoa vikali tangazo hilo la Netanyahu. Marekani inasisitiza kwamba operesheni ya kijeshi kwenye mji huo itakuwa na athari kubwa hasa kwa watu waliojihifadhi kwenye mji huo, baada ya kukimbia mapigano katika Ukanda wa Gaza. 

"Leo nimepokea ripoti ya kina juu ya mazungumzo ya Cairo na tunayafanyia kazi mara kwa mara ili kufikia malengo yetu, kwanza kabisa kuachiliwa mateka wetu wote na kupata ushindi kamili dhidi ya Hamas. Ili kupata ushindi huu tunalazimika kuingia ndani ya Rafah na kuvimaliza vikosi vya kigaidi vilivyoko huko. Tutafanya hivyo. Tayari tarehe imepangwa." Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ametoa ujumbe wake mfupi kwa njia ya video jana Jumatatu, ingawa hakuweka wazi ni lini hasa wataanza operesheni hiyo.

Mipango ya Israel ya kuivamia Rafah kijeshi imekuwa ikipingwa vikali na washirika wake wa kimataifa kutokana na kuongezeka kwa mzozo wa kibinaadamu katika Ukanda wa Gaza.

Marekani yaendelea kupinga uvamizi wa Israel katika mji wa Rafah

Mara baada ya tangazo hili, Marekani ambayo pia imekuwa ikipinga uvamizi huu ikasema kupitia msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Matthew Miller kwamba hawajabadilisha msimamo wao kuhusu mpango huo wa Israel wa kuivamia kikamilifu Rafah iliyoko kusini mwa Gaza.

Soma pia: White House yasema raia wa Rafah wanahitaji kulindwa

Rais Joe Biden amekuwa mstari wa mbele kupinga uvamizi wa Israel kwenye mji wa Rafah unaokaliwa na Wapalestina walioyakimbia mapiganoPicha: Brendan Smialowski/AFP

Tangu mwezi Februari, Marekani ilionya juu ya uvamizi huo ikisema utaibua mzozo mkubwa wa kibinaadamu kwa kuwa zaidi ya Wapalestina milioni 1 wamejihifadhi kwenye mji huo wakiyakimbia mapigano yanayoendelea katika maeneo mengine ya Gaza iliyozingirwa na wanajeshi wa Israel.

Soma pia:Mashambulizi makali ya Israel yailenga Rafah 

Miller amesema, Marekani haiangalii tu upande mmoja wa Israel kuwasilisha mpango wao, bali wanaangazia pande zote na hasa kwa kuwa tayari wamewaeleza wazi  kwamba wanaamini kuna namna bora zaidi ya kufikia lengo la kuvisambaratisha kabisa vikosi vya Hamas vilivyosalia Rafah.

Hamas: Watu zaidi ya 33,000 wafa kutokana na vita

Kulingana na Wizara ya Afya inayoratibiwa na Hamas katika Ukanda wa Gaza, idadi ya Wapestina waliokufa hadi sasa kutokana na mapigano imepindukia 33,200 na karibu 76,000 walijeruhiwa tangu vita hivyo vilipoanza Oktoba 7 mwaka uliopita.

Na huko mjini Cairo, taarifa zinasema wapatanishi kwenye  mzozo huu wamewasilisha pendekezo la makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kwa wawakilishi wa Hamas na Israel.

Watoto wa Kipalestina waliokimbia makazi yao kutokana na vita wakiwa wamekaa mbele ya hema la muda kwenye kambi huko Rafah, Machi 14, 2024 katikati ya vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas.Picha: Mohammed Abed/AFP

Makubaliano hayo, yatakayotekelezwa kwa wiki sita, yatajumuisha usitishwaji wa mapigano na makubaliano ya Hamas kuwaachia mateka 40 wa Israel na Israel kuwaachia wafungwa karibu 700 wa Kipalestina wanaozuiwa nchini humo.

Soma pia: Qatar yasema ina matumaini katika mazungumzo mapya ya Doha

Pendekezo hilo liliwasilishwa kwa wawakilishi wa Hamas na Israel kwenye awamu ya karibuni zaidi ya mazungumzo mjini Cairo, hii ikiwa ni kulingana na afisa mmoja ambaye hakutaka kutambulishwa.

Miongoni mwa wafungwa wa Kipalestina watakaoachiliwa ni pamoja na watuhumiwa wa mauaji ya Waisrael wakati Hamas ilipoishambilia Israel. Hamas nao watatakiwa kuwasilisha orodha ya mateka itakaowaachilia, pamoja na wafungwa wanaotaka waachiliwe.

Hamas imesema inalipitia pendekezo hilo.

Katika hatua nyingine, Uturuki imetangaza vikwazo vya kibiashara kwa baadhi ya bidhaa nchini Israel ambazo ni pamoja na mabati, chuma cha pua, vifaa vya ujenzi na mbolea kutokana na hatua zake katika Ukanda wa Gaza, baada ya kukataa ombi la Uturuki la kuungana na ndege nyingine za mizigo kuangusha misaada Gaza na kuahidi kuendelea kuchukua hatua hadi Israel itakapotangaza kusitisha mapigano na kuruhusu uingizwaji wa misaada bila ya vizuizi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW