Marekani, Iran zaendelea 'kutwangana'
16 Julai 2026
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilidai kuishambulia meli moja ya mafuta iliyokuwa ikijaribu kutia nanga kwenye bandari moja ya Iran siku ya Jumatano (Julai 15), baada ya manahodha wa meli hiyo kupuuzia onyo la Kamandi hiyo.
Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, Kamandi hiyo ilisema meli hiyo inayopeperusha bendera ya Curacao ilikuwa ikipita kwenye bahari inayotambuliwa kimataifa ikielekea kwenye Kisiwa cha Kharg, ambacho ni kituo muhimu kwa sekta ya mafuta ya Iran.
Kwa mujibu wa CENTCOM, meli hiyo ilikuwa inakiuka mzingiro wa baharini uliowekwa na Marekani dhidi ya Iran, na kwamba ndege ya kijeshi ilihusika kwenye kuishambulia meli hiyo na kwamba sasa haielekei tena Iran.
Kurudi kwa mzingiro wa Marekani
Tangu Jumanne (Julai 14), Washington imerejesha kile ikiitacho mzingiro dhidi ya bandari za Iran kuzizuwia meli za kibiashara kuingia na kutoka kwenye Jamhuri hiyo ya Kiislamu, ikidai ndiyo njia pekee ya kuilazimisha Tehran kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz.
Mlango Bahari huo muhimu kabisa kwa usafirishaji wa nishati ulimwenguni, kwa sasa umefungwa tena na Jeshi la Walinda Mapinduzi la Iran kwa muda usiojulikana kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani dhidi ya Iran licha ya kuwapo kwa mkataba wa kusitisha mapigano baina yao.
Marekani iliwahi kuweka mzingiro kama huo kuanzia katikati mwa mwezi Aprili lakini ikauondosha katikati ya Juni kama sehemu mojawapo ya utekelezaji wa vipengele vya makubaliano ya muda kukomesha vita hivyo vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mwishoni mwa mwezi Februari.
Kwenye mashambulizi mengine, jeshi la Marekani linaripotiwa kuyashambulia tena maeneo ya kusini mwa Iran, ambapo makombora yameanguka kwenye miji ya Sirik na Qeshm, kwa mujibu wa shirika la habari la Iran, IRIB.
Makombora mengine yameangukia karibu na hospitali ya Ahvaz, inayowatibu wagonjwa wa saratani na kulazimisha wagonjwa kuhamishwa kwa muda.
Iran yazishambulia Bahrain, Kuwait, Jordan
Kwa upande wake, Iran nayo iliendelea na mashambulizi yake dhidi ya vituo vya kijeshi na maslahi ya Marekani kwenye mataifa ya Ghuba usiku kucha wa Jumatano.
Huko Kuwait, mamlaka zilisema jeshi lake limefanikiwa kuzidunguwa droni 21 na makombora manne kutokea Iran, huku milio ya ving'ora ikisikika kote kwenye mji mkuu, Bahrain.
Kupitia mtandao wa kijamii wa X, jeshi la Kuwait limesema mapema leo kwamba lilikuwa linakabiliana na mashambulizi ya droni kutokana na kile lilichokiita "uchokozi usio sababu wa Iran."
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kuwait imewatolea wito raia kuwa watulivu na kuelekea kwenye maeneo salama yaliyo karibu yao.
Jeshi la Iran limerusha makombora pia kuelekea Bahran na Jordan kwenye vituo vya kijeshi vya Marekani.
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, Hossein Mohebbi, amesema mashambulizi ya sasa yanalenda kuimalizia miundombinu ya kijeshi ya Marekani kwenye eneo la Ghuba na kwamba awamu inayofuatia itaanza karibuni.