1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Israel zakutana na nchi za Kiarabu dhidi ya Iran

28 Machi 2022

Wanadiplomasia wakuu kutoka Marekani na nchi nne za kiarabu wamekutana nchini Israel, katika ishara ya ushirikiano dhidi ya Iran.

Israel Sde Boker |  Gipfeltreffen in Israels Wüste
Picha: Jacquelyn Martin/AP/picture alliance

Pia wametumia mkutano huo wa kilele kuishinikiza mwenyeji wao Israel, kufufua juhudi ambazo zimekwama kwa muda mrefu za kusaka amani na Wapalestina.

Wakikamilisha mkutano wao wa siku mbili, mahali ambapo muanzilishi wa taifa hilo David Ben-Gurion alizikwa, Israel imesema mikutano kama hiyo itafanyika kuhusu masuala mengine kama biashara na usalama kati yao na nchi hizo za kiarabu.

Viongozi wa Israel,Misri na UAE wakutana pamoja kwa mara ya kwanza

Waziri wa mambo ya nje wa Israel Yair Lapid akiwa na wenzake wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Morocco na Misri, amesema ushirikiano huo mpya unatishia na vilevile unawazuia maadui zao hususan Iran na washirika wao.

Israel na baadhi ya nchi za kiarabu zina wasiwasi kuhusu mkataba wa silaha za nyuklia wa Iran, kwamba unaweza kuiacha nchi hiyo na uwezo wa kutengeneza mabomu na kuimarisha makundi ya wapiganaji ambayo ni washirika wake.

Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett (Kulia) wakizungumza baada ya mkutano katika ofisi ya Bennett mjini Jerusalem Machi 27, 2022.Picha: ABIR SULTAN/UPI/IMAGO

Juhudi za kuufufua mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran

Marekani na nchi nyingine zenye nguvu zaidi ulimwenguni zinajaribu kuufufua mkataba kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran kama mbadala bora. Lakini waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken amewahakikishia washirika wa nchi yake katika eneo la Mashariki ya Kati ushirikiano wao endapo juhudi hizo za kidiplomasia zitashindwa.

Marekani, Israel waijadili Iran ikigoma kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia

Akiyasifia makubaliano hayo, Blinken ameongeza kusema kuwa  ni sharti waeleze wazi kwamba mikataba hiyo ya amani ya kikanda, si mbadala wa juhudi zinazoendelea za kusaka amani kati ya Israel na Wapalestina.

"Kwa hivyo miongoni mwa masuala tuliyojadili leo ni namna nchi zinazohusika kwenye mkataba wa Abraham na nyingine ambazo kwa muda mrefu zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia na Israel, zinavyoweza kuisaidia mamlaka ya Wapalestina na Wapalestina kwa njia bora na kuleta matokeo chanya katika maisha ya kila siku ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi na Gaza," amesema Blinken.

Nchi za Kiarabu zarejesha uhusiano na Israel

Antony Bennet asema kwa sasa mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Israel na nchi nne za Kiarabu wanaweza kusimama pamoja na wazungumze, jambo ambalo halikuwa rahisi kufanyika miaka ya zamani. Picha: Jacquelyn Martin/AP/picture alliance

Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Morocco, zilirejesha uhusiano  na Israel mwaka 2020 chini ya juhudi za upatanisho za mpango wa Marekani ujulikanao kama Mkataba wa Abraham.

Bennet akutana na mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi Mohammed bin Zayed Al Nahyan

Mnamo mwaka 1979, Misri ilikuwa nchi ya kwanza ya kiarabu kuweka makubaliano ya amani na Israel.

Sawa na nchi za kiarabu, Marekani pia inataka suluhisho la mataifa mawili ambapo Wapalestina watapata utaifa sawa na Israel. Mazungumzo kuhusu juhudi hizo yalikwama mwaka 2014.

”Kama ilivyo kwa majirani na katika muktadha huu wa Marekani kama marafiki, tutashirikiana pamoja kukabili changamoto za kiusalama na vitisho, vikiwemo kutoka Iran na wapambe wao” amesema Blinken.

Waziri wa mambo ya nje wa Bahrain Abdullatif Al. Zayani aliyataja mazungumzo yao kuwa muhimu kuyakabili makundi yanayoiunga mkono Iran kwa mfano Hezbollah.

(Rtre)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW