1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Israel zazidi kuwaangamiza makamanda wa IRGC

7 Aprili 2026

Makamanda wa jeshi la Mapinduzi la Iran, IRGC wameuawa huku mashambulizi ya Israel na Marekani yakiongezeka Tehran. Iran nayo imeendeleza mashambulizi Israel na Ghuba huku ikikataa mapendekezo ya Marekani kumaliza vita.

Iran, Tehran 2026 | Mkuu wa ujasusi wa IRGC, Majid Khademi, katika mahojiano.
Brugedia Jenerali Majid Khademi, alikuwa mkuu Intelijensia wa Jeshi la Walinzi wa Mapinfuzi, alieuawa katika mashambulizi ya Israel mjini Tehran Jumatatu.Picha: Iranian Supreme Leader's Office/ZUMA/picture alliance

Kikosi cha Ulinzi wa Mapinduzi ya Iran, IRGC, kimesema mkuu wake wa idara ya ujasusi, Meja Jenerali Majid Khademi, aliuawa Jumatatu huku Iran ikishambulia eneo la Tel Aviv, na muda wa mwisho uliowekwa na Marekani kwa Tehran kufikia makubaliano ukikaribia.

Baadaye, jeshi la Israel liliripoti kifo cha kiongozi mwingine wa juu wa kijeshi — mkuu wa kikosi maalum cha Quds Force — likisema aliuawa Tehran Jumapili. Kamanda Asghar Bagheri alihusishwa na mashambulizi yaliyolenga Waisraeli na Wamarekani duniani kote.

Taarifa hizo zilikuja huku watu wasiopungua 19 wakiuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel karibu na Tehran, kulingana na shirika la habari la serikali ya Iran IRNA.

Maeneo ya Shahriar na Baharestan yalishambuliwa, na majengo mawili ya ghorofa tatu yakaharibiwa kabisa kusini-magharibi mwa mji mkuu. Miili kadhaa ilipatikana kwenye vifusi.

Shirika la habari la Tasnim liliripoti kuwa watoto sita wenye umri chini ya miaka 10 — wavulana watatu na wasichana watatu — waliuawa katika mashambulizi hayo.

Iran pia iliripoti shambulio jipya kwenye miundombinu ya gesi katika Ghuba ya Uajemi. Mlipuko uliripotiwa karibu na kiwanda cha kusafisha gesi katika mji wa pwani wa Asaluyeh, kitovu cha sekta ya gesi nchini humo. Mashambulizi zaidi yalilengwa kwenye kiwanda cha kemikali Marvdasht karibu na Shiraz, yakisababisha moto uliodhibitiwa baadaye.

Timu za uokoaji za Hilali Nyekundu zilikuwa zikitafuta waathirika katika eneo lililoshambuliwa na mashambulizi ya anga ya pamoja ya Marekani na Israel kwenye majengo ya makazi mjini Tehran, siku ya Jumatatu, Aprili 6, 2026.Picha: Iranian Red Crescent/UPI Photo/IMAGO

Iran yaishutumu IAEA kwa ukimya

Tehran ililikosoa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani, IAEA, kwa kushindwa kulaani mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani na Israel karibu na kinu pekee cha nyuklia cha Iran huko Bushehr.

Katika barua kwa mkurugenzi mkuu Rafael Grossi, mkuu wa shirika la nishati ya atomiki la Iran Mohammad Eslami alisema kushindwa kwa IAEA kulaani mashambulizi hayo kunaweza kuwahamasisha "washambuliaji” kuendelea na mashambulizi.

Katika shambulio la Jumamosi karibu na kinu hicho, mfanyakazi mmoja wa usalama aliuawa na jengo la pembeni kuharibiwa, ingawa kinu chenyewe hakikupata uharibifu.

Shinikizo la Marekani laendelea

Marekani na Israel zilianza mashambulizi dhidi ya Iran Februari 28. Iran ilijibu kwa makombora dhidi ya Israel na nchi za Kiarabu katika Ghuba, na kusababisha usafirishaji kusimama karibu kabisa katika Mlango wa Hormuz.

Rais wa Marekani Donald Trump ametoa mara kadhaa — na kuchelewesha — muda wa mwisho wa kufunguliwa tena kwa njia hiyo muhimu ya majini. Katika ujumbe mkali, alionya kuwa Iran "itaishi katika mateso makubwa” ikiwa haitafungua njia hiyo kufikia Jumanne jioni.

Hata hivyo, Iran ilisema imewasilisha mapendekezo ya kumaliza mzozo huo kupitia wapatanishi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Esmail Baghaei alisema madai ya Marekani ni makubwa kupita kiasi na hayakubaliki.

Rais Donald Trump amesema madaraja na vituo vya umeme nchini Iran vitaangamizwa kuanzia saa sita za usiku endapo Tehran haitafikia makubaliano kufikia muda huo.Picha: Yuri Gripas/abaca/picture alliance

Chuo kikuu chashambuliwa Tehran

Chuo maarufu cha Sharif University of Technology kilishambuliwa kwa mabomu, siku chache baada ya taasisi nyingine muhimu pia kulengwa.

Kituo cha data cha chuo hicho — kinachotumiwa na walimu, wanafunzi na kampuni changa — kiliharibiwa kabisa. Wahitimu wake wanajumuisha mwanahisabati mashuhuri Maryam Mirzakhani.

Shirika la Amnesty International lilisema mashambulizi dhidi ya vyuo yana athari kubwa kwa jamii ya Iran, likieleza kuwa watu wengi wameguswa bila kujali misimamo yao ya kisiasa.

Mashambulizi yaenea Israel na Ghuba

Nchini Israel, makombora yalipiga eneo la Tel Aviv, huku vituo 30 vya athari vikiripotiwa na watu kadhaa kujeruhiwa. Uharibifu mkubwa uliripotiwa katika mji wa Ramat Gan.

Iran pia iliendelea kushambulia nchi za Ghuba, ikiwemo Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu, ambapo mtu mmoja alijeruhiwa.

Timu za manispaa zikifanya usafi na kuondoa mabaki baada ya vipande vya makombora kutoka mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran kupiga maeneo ya Tel AvivPicha: Saeed Qaq/Anadolu/picture alliance

Katika emarati ya Fujairah, jengo la kampuni ya mawasiliano lilishambuliwa na droni. Wizara ya ulinzi ya UAE ilisema ilidungua makombora 12 ya balistiki, makombora mawili ya cruise na droni 19.

Kuwait iliripoti majeruhi sita kutokana na mabaki ya makombora yaliyodunguliwa, huku Saudi Arabia ikisema ilidungua droni mbili. Jordan nayo iliripoti watu wawili kujeruhiwa baada ya matukio yanayohusiana na mashambulizi hayo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW