Marekani itajiondoa kwenye mpango wa nyuklia wa Iran?
13 Oktoba 2017Mpango huo uliofikiwa na Iran na nchi nyingine sita zenye nguvu duniani mnamo mwaka 2015 baada ya miaka zaidi ya kumi ya mazungumzo magumu, sasa umo mahala pabaya. Trump anatarajiwa kukataa kuuidhinisha mpango huo kwa sababu anaona kuwa ni mbaya ambao haukidhi maslahi ya taifa la Marekani. Trump anakabiliwa na shinikizo kubwa jinsi anavyozingatia hatua ya kuukiuka mpango huo inayochukuliwa sawa na kupuuza tahadhari kutoka ndani na nje ya utawala wake kwamba kufanya hivyo kutaleta hatari ya kudhoofisha uaminifu wa Marekani kwa nchi za nje.
Rais huyo wa Marekani mara mbili alishaidhinisha mkataba huo wa kimataifa wa Iran lakini kwa mujibu wa wasaidizi wake wanasema Trump mara hii anasita kuuidhinisha kwa mara ya tatu. Urusi imetoa angalizo kwa Marekani kwamba kuutelekeza mpango huo wa nyuklia wa Iran litakuwa ni pigo kubwa kwa uhusiano ya kimataifa na juhudi za kuzuia ongezeko la kuenea silaha za nyuklia. Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov, alipozungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif kwa njia simu, alimueleza kuwa nchi yake inaunga mkono kikamilifu mpango wa nyuklia wa Iran, unaoitwa "Mpango imara wa Utekelezaji wa Pamoja" "Joint Comprehensive Plan of Action" (JCPOA).
Makubaliano hayo yalitiwa saini baina ya Iran na nchi za Marekani, Ujerumani, Uingereza Ufaransa, Urusi na China katika mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Ulaya. Wahusika wote wanauunga mkono kwa dhati mpango huo na wanasema kuwa Iran imeendelea kuheshimu ahadi yake inayoazimia kuizuia nchi hiyo kuendelea na mpango wake wa nyuklia. Wapinzani wa mpango huo wanasema unabana nafasi ya jitihada za kupinga ushawishi wa Iran unaoongezeka katika Mashariki ya Kati.
Mwenyekiti wa kamati ya usalama wa ndani nchini Marekani Michael MacCaul ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba anadhani rais Trump hataitoa Marekani kwenye mpango huo bali hatafuata yale yaliyothibitishwa hapo awali. Spika wa bunge la Iran Ali Larijani amesema iwapo Marekani itajitoa kwenye mpango huo bila shaka ndio utakuwa mwisho wake na ulimwengu mzima utakabiliwa na vurugu.
Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE/AFPE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman