1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiMarekani

Marekani Itapunguza adhabu kwa washtakiwa wa ugaidi?

27 Oktoba 2023

Watu wanaopatikana na hatia ya uhalifu unaohusiana na itikadi kali nchini Marekani, hukabiliwa na vifungo vya muda mchache kuliko wale waliopatikana na hatia katika kesi za ugaidi wa kimataifa.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Hayo yametajwa katika ripoti mpya  iliyojikita- katika matokeo ya mamia ya kesi za jinai kote nchini Marekani.

Utafiti huu wa kwanza na wa aina yake ambao umeendeshwa na watafiti wa masuala ya ugaidi katika Chuo Kikuu cha Maryland, unakuja baada ya maafisa na watafiti wa shirikisho nchini Marekani kubainisha mara kadhaa kuwa watu wenye itikadi kali nchini humokama vile makundi ya watu wenye mrengo mkali wa kulia na yale yanayoipinga serikali, ndio tishio kubwa la ugaidi kwa Marekani.

Taarifa hii inaibuliwa huku uchunguzi wa matokeo ya Kesi za Januari 6, zikiwemo zile za makundi ya Walinzi wa Viapo "Oath Keepers" na Proud Boys kuhukumiwa kifungo cha miaka michache kuliko kile kilichotakiwa na waendesha mashtaka pamoja na miongozo ya hukumu katika kesi kama hizo.

Rais Joe Biden amesisitiza wasiwasi wake kuhusu ugaidi wa ndani na kuutaja kwa kile alichosema ni "doa katika moyo wa Marekani na tishio kubwa" linaloikabili nchi hiyo.

Soma pia:Watuhumiwa wawili wa Westgate wakutwa na hatia, moja aachiwa

Lakini bado uchambuzi mpya unaonyesha kwamba kwa wastani, watu wenye msimamo mkali nchini Marekani hupewa adhabu isiyokuwa kali.

Shirin Sinnar, profesa katika shule ya sheria ya Stanford, ambaye hakuhusika katika utafiti huo lakini ameukagua kwa makini kwa ombi la AP anasema utafiti huu ni muhimu katika kudhibitisha kile ambacho wengi wamekuwa wakibishana kwa muda mrefu.

Miaka 25 tangu mashambulizi ya kigaidi Nairobi na Dar

03:33

This browser does not support the video element.

Alisema kuwa kesi za ugaidi za kimataifa zinahukumiwa kwa ukali zaidi kuliko kesi za ugaidi wa ndani, hata wakati vitendo vikilingana, na kwamba tofauti hizi zinatokana na mkanganyiko uliopo katika sheria za Marekani na upendeleo katika utekelezaji.

Watafiti hao katika Chuo Kikuu cha Maryland wanaofuatilia masuala ya ugaidi (START), walichunguza kesi za uhalifu uliofanywa kote Marekani kati ya mwaka 2014 na 2019 zilizoanzishwa dhidi ya watu wenye msimamo mkali wa kisiasa, kijamii, kiuchumi au kidini.

Kifungo kirefu kwa washtakiwa wa kimataifa

Kesi za ugaidi wa kimataifa zilifafanuliwa na watafiti kama zile ambazo washtakiwa walikuwa na uhusiano, kushirikiana au kuunga mkono vuguvugu au makundi ya kigaidi yaliyopo nje ya Marekani, huku kesi za ndani zikiwahusisha washtakiwa waliojiunga na vikundi ambavyo kimsingi huendesha shughuli zao ndani ya Marekani.

Utafiti huo ulifuatilia kesi 344, ambapo kesi 118 zilikuwa za kimataifa na kesi 226 za ndani, na kubainisha kuwa tofauti husababishwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na mashtaka ambayo hufunguliwa na waendesha mashtaka wa shirikisho, sheria zilizopo na hukumu inayotolewa na majaji.

Jina la mhanga wa shambulio la kigaidi Marekani likipepea kwenye benderaPicha: Spencer Platt/Getty Images

Utafiti wa START uliweka bayana tofauti kubwa ya vifungo katika aina fulani za kesi hasa pale washtakiwa walipopanga mashambulizi ya kikatili ambayo hatimaye yalifeli au kuzimwa.

Washtakiwa wa ugaidi wa kimataifa walihukumiwa kifungo cha wastani miaka 11 na miezi miwili,  ikilinganishwa na mwaka 1 na miezi 6 kwa washtakiwa wa ugaidi wa ndani.

Soma pia:Wanaume watatu wafunguliwa mashtaka ya ugaidi Ubelgiji

Ama katika kesi za vurugu zilizosababisha majeraha, washtakiwa wa ndani walihukumiwa kwa wastani wa miaka 8 na miezi 6 dhidi ya miaka 34 na nusu kwa washtakiwa wa kimataifa.

Si hayo tu, hata masharti ya usimamizi huko jela yalidhihirisha utofauti baina ya makundi hayo mawili.

Lakini watafiti wa START wanaeleza kuwa licha ya yote hayo, ushahidi ni kwamba uwezekano wa kurejea makosa ya awali ni takriban asilimia 50 kwa watu wenye msimamo mkali wa ndani ikiwa ni sawa na wahalifu wote wa shirikisho.

Lakini kiwango hicho ni chini kabisa kwa washtakiwa wa ugaidi wa kimataifa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW