Marekani itayari kufanya mashambulizi zaidi Syria
11 Aprili 2017Haya ni katika harakati za kujadili jinsi watakavyomuondoa madarakani rais wa Syria Bashar al-Assad, saa chache kabla waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson kusafiri kuelekea Urusi, taifa kubwa pekee linalomuunga mkono Assad.
Mawaziri hao wa nchi za nje za G7 wanafanya mazungumzo na wenzao kutoka Uturuki, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu, Jordan na Qatar wote hawa wakiwa wanapinga utawala wa Assad, ili kuzungumzia mzozo wa ndani ya Syria uliodumu kwa kipindi cha miaka sita.
Mazungumzo haya yamekuja wakati ambapo Marekani kupitia Msemaji wa ikulu ya White House Sean Spicer, imeonya kwamba iko tayari kufanya mashambulizi zaidi ya kijeshi nchini Syria iwapo wanajeshi wa Syria wataendelea kutumia zana za kemikali, licha ya Urusi kupinga hatua hiyo. Spicer amesema kwamba Marekani imejitolea kuhakikisha matumizi ya silaha hizo yanakoma.
Mataifa hayo ya G7 yatafakari kuiongezea vikwazo Urusi
"Sio Syria tu, lakini dunia iliona wiki iliyopita rais atakayefanya maamuzi ya haki kuhusiana na masuala kama hayo," alisema Spicer, "na nitawaambia, jawabu ni kwamba ukimuua mtoto kwa silaha ya sumu, ukiwapiga mabomu watu wasio na hatia, nadhani rais huyu atakujibu. Hilo si jambo linalokubalika," aliongeza msemaji huyo.
Afisi ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa May, imetoa taarifa iliyosema kwamba, kiongozi huyo alizungumza na rais wa Marekani Donald Trump jana na wakakubaliana kwamba upo uwezekano wa kuishawishi Urusi kuacha kuiunga mkono Syria.
Uingereza na Canada pia zilisema vikwazo dhidi ya Urusi vinaweza kuongezwa iwapo taifa hilo litaendelea kumuunga mkono Assad.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel naye ameunga mkono hatua ya kuhakikisha Urusi inajitenga na Assad akidai kwamba hiyo ndiyo njia itakayohakikisha kwamba Putin yuko tayari kushirikiana nao katika kupata suluhu la kisiasa.
"Huu ndio wakati mwafaka wa kuzungumzia juhudi za kupatikana kwa amani nchini Syria kati yetu jamii ya kimataifa, pamoja na Urusi, Iran, Saudi Arabia, Ulaya na Marekani," alisema Gabirel, "ili kuzuia machafuko ya kijeshi kuongezeka tunastahili kufanya hivi," aliongeza waziri huyo.
Tillerson kuzuru Urusi baada ya mkutano wa G7
Juhudi hizi za G7 kutaka kuwa nguvu moja dhidi ya Assad zinakuja mbele ya ziara wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson nchini Urusi, hiyo ikiwa ni ziara ya kwanza ya afisa wa ngazi ya juu katika uongozi wa rais Trump.
Tillerson anakabiliwa na kibarua chake cha kwanza kigumu zaidi katika masuala ya diplomasia ya kimataifa, kwani atakuwa anakabiliana na Urusi ambayo imekanusha madai ya Marekani kwamba wanajeshi wa Syria walitumia zana za kemikali wiki iliyopita.
Mbali na Syria, mkutano wa G7 leo hii utazungumzia Libya pia ambapo watu wanaoendesha biashara ya kuwaingiza wahamiaji barani Ulaya kimagendo wanafanya hivyo kwa kukiuka haki za binadamu na wanashindana na serikali na wanamgambo kuwania mamlaka.
Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga