Marekani, Japan na Korea zaweka makubaliano mapya ya usalama
18 Agosti 2023Kwa mujibu wa afisa mmoja wa ngazi za juu katika serikali ya Rais Joe Biden wa Marekani aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mataifa hayo matatu yamekubaliana kuwa ujumbe mmoja wakati wa tishio ama mgogoro. Afisa huyo ameongeza kuwa mpango huo haukiuki haki ya kila taifa ya kujilinda chini ya sheria ya kimataifa wala haubadilishi makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa pande mbili kati ya mataifa mawili ya Marekani na Japan na Marekani na Korea Kusini. Marekani ina zaidi ya wanajeshi 80,000 katika mataifa hayo mawili.
Soma pia: Marekani, Japan na Korea Kusini zalaani hatua ya Korea Kaskazini kurusha kombora
Lengo la Biden ni kwa mataifa hayo kuimarisha usalama na ushirikiano wa kiuchumi
Kongamano hilo ni la kwanza kuandaliwa na Biden chini ya urais wake katika eneo la mapumziko la Camp David. Lengo la Biden katika mkutano huo wa kilele ni kuwashawishi washirika hao wa karibu wa Marekani katika bara Asia kuimarisha usalama na ushirkiano wa kiuchumi na kila mmoja.
Chini ya Uongozi wa Kishida na Yoon, Japan na Korea Kusini zimeanza kukaribiana tena
Wapinzani hao wa kihistoria wamegawanywa na maoni tofauti kuhusu historia ya vita vya pili vya dunia na utawala wa kikoloni wa Japan katika rasi ya Korea kutoka mwaka 1910 hadi 1945.
Lakini chini ya uongozi wa Kishida na Yoon, mataifa hayo mawili yameanza kukaribiana tena huku viongozi hao wawili wa kihafidhina wakikabiliana na changamoto za pamoja za kiusalama kutoka kwa Korea Kaskazini na China.
Soma pia: Korea Kaskazini yafanya jaribio la kombora la masafa marefu
Viongozi wote wawili wameghadhabishwa na kuongezeka kwa majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini na mazoezi ya kijeshi ya China karibu na kisiwa cha Taiwan kinachojitawala ambacho kinadaiwa na China kama sehemu ya eneo lake pamoja na hatua nyingine za uchokozi.
Marekani, Japan na Korea Kusini kuelezea teknolojia ya mawasiliano ya dharura
Wakati wa mkutano huo wa kilele, viongozi hao watatu, pia wanatarajiwa kueleza kwa kina teknolojia ya mawasiliano ya dharura ya pande tatu wakati wa mzozo na kutoa taarifa kuhusu hatua ambazo nchi hizo zimechukuwa za kushirikishana taarifa za onyo la mapema kuhusu kurushwa kwa makombora kutoka Korea Kaskazini. Matangazo mengine yanayotarajiwa kutoka kwa mkutano huo ni pamoja na mipango ya kupanua ushirikiano wa kijeshi kuhusu ulinzi wa makombora na kulifanya kongamano hilo kuwa hafla ya kila mwaka.
Mshauri wa usalama wa kitaifa wa Biden Jake Sullivan, amesema viongozi hao leo, pia watajitolea kwa mchakato wa mipango ya miaka mingi ya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.