Marekani, Jordan zaapa kuimarisha ushirikiano
20 Julai 2021Ziara hiyo katika Ikulu ya Rais ilikuwa ya kwanza kwa kiongozi wa taifa la Kiarabu tangu Biden aingie madarakani miezi sita iliyopita, na ilitumika kuonyesha uungaji mkono wa Marekani kwa Jordan kufuatia madai ya njama ya kuupindua uongozi wa mfalme huyo iliyofanywa na kaka yake kwa baba.
Biden alimshukuru Mfalme Abdullah II kwa kudumisha uhusiano wa kimkakati na Marekani kwa miaka mingi. Rais huyo wa Marekani ameweka mwelekeo mkubwa wa sera zake za nje katika suala la China na Urusi anakabiliwa na changamoto kadhaa katika suala la Mashariki ya kati.
Anakabiliwa na ongezeko la mashambulio yanayofanywa dhidi ya wanajeshi wa Marekani huko Iraq na Syria, mashambulio yanayofanywa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran lakini wakati huo huo serikali ya Biden inajaribu pia kuwasogeza Wairan kurudi kwenye meza ya mazungumzo kufufua makubaliano ya kimataifa ya Nyuklia yaliyopigwa kikumbo na mtangulizi wake Donald Trump.
Mfalme Abdullah wa II alizungumzia changamoto ambazo nchi yake inakabiliana nazo katika kukuza amani ya Mashariki ya Kati. Ni kiongozi aliyekuwa kwenye hali ngumu ya uhusiano na rais wa zamani wa marekani Donald Trump ambaye alikuwa akimtazama kama kiongozi aliyekuwa akidhoofisha makubaliano ya amani kati ya Waisrael na Wapalestina kutokana na azimio lake la mwaka 2017 la kuitangaza Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.
afp, dpa, ap, reuters