Marekani, Korea Kusini waanza mazoezi ya kijeshi
22 Agosti 2022Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Korea Kusini amethibitisha kuanza kwa mazoezo hayo ya kijeshi kama ilivyopangwa, lakini hakutoa maelezo zaidi juu ya idadi ya wanajeshi watakaohusika na vifaa gani vya kijeshi vitakavyotumika. Hata hivyo vyombo vingine vya habari vimeripoti kwamba mazoezi hayo yatahusisha vifaru, ndege na meli za kivita na maelfu ya wanajeshi.
Rais wa Korea Kusini pamoja na masuala mengine amesema mazoezi hayo yatakuwa mwanzo wa serikali kujipanga upya maandalizi yake ya kukabiliana na dharura kwa kuzingatia mabadiliko yaliyopo kwenye mfumo mzima wa vita ulimwenguni.
Amesema "Vita katika nyakati hizi ni tofauti kabisa na vile vya zamani. Maadui watafanya mashambulizi ya mtandaoni, kwenye miundombinu ya kitaifa ya habari na mawasiliano na kushambulia maeneo muhimu vya viwanda kama vile bandari, viwanja vya ndege na vinu vya nishati ya nyuklia; vifaa vya teknolojia ya juu na mifumo ya ugavi wa malighafi ili kupunguza uwezo wetu wa kupigana vita. Zoezi hili la Ulchi litakuwa mwanzo kwa serikali kupanga upya maandalizi yake ya dharura kulingana na mabadiliko ya mifumo ya vita"
Marekani ina wanajeshi karibu 28,500 waliopiga kambi Korea Kusini, ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na vitisho kutoka kwa Korea Kaskazini, iliyojitangaza kuwa taifa lenye nguvu kinyuklia.
Soma Zaidi: Marekani na Korea Kusini zatafakari kutanua Luteka za Kijeshi
Luteka hizo zilizopewa jina Ulchi Freedom Shield zinahusisha mafunzo ya kompyuta, mazoezi ya pamoja ya kivita na mazoezi makubwa ya kuwalinda raia. Zinatarajiwa kukamilika Septemba Mosi. Seol hata hivyo inajiandaa na ukosoaji mkali kutoka kwa Korea Kaskazini baada ya kiongozi wa taifa hilo mara kwa mara kuituhumu Marekani kwa kuandaa uvamizi kupitia mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi na Korea Kusini.
Washington na Seoul hata hivyo wanakana shutuma hizo na kusisitiza kwamba mazoezi hayo yana nia ya kuboresha uwezo wa kujilinda.
Wasiwasi wa kikanda umezidi kuongezeka mwaka huu baada ya majaribio ya mfululizo ya makombora yaliyofanywa na Korea Kaskazini.
Lakini pia mazoezi hayo yalipunguzwa katika miaka ya karibuni ama kufutwa kabisa kutokana na sababu za kidiplomasia na janga la UVIKO-19. Mazoezi ya majira ya joto ya mwaka 2018 yalifutwa kabisa ikiwa ni sehemu ya jaribio la kutafuta fursa ya mazungumzo juu ya mipango ya nyuklia ya Korea Kaskazini.
Soma Zaidi: Marekani na Korea Kusini zapanga kusitisha Luteka za kijeshi
Hata hivyo mazungumzo hayo yamesimama tangu, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump kushindwa kuafikiana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, walipokutana katika mkutano wa kilele huko Vietnam, Februari 2019. Kim hatimaye aliapa kujiimarisha zaidi kinyuklia licha ya vitisho vya Marekani, hasa baada ya taifa hilo kuyakataa masharti ya Korea Kaskazini ya kuondoa kiasi kikubwa cha vikwazo viliyozorotesha vibaya uchumi wa taifa hilo.
Mashirika: APE/DPAE